Maendeleo ni mchakato mrefu unaogharimu muda, rasilimali fedha na utaalam.
Kote duniani maendeleo hupimwa katika misingi ya kuimarika na kuboreka kwa huduma za kijamii.
Ili kufikia maendeleo, ni lazima pawepo mikakati madhubuti na endelevu ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya muda mfupi, kati na mrefu.
Tangu ilivyoingia madarakani Novemba 5, 2015, Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imejipambanua kuwa na nia thabiti ya kujenga Tanzania mpya, Tanzania ya watu wanaochapa kazi.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Rais Magufuli amefanya mengi ya kupigiwa mfano katika maendeleo ya sekta za afya, elimu, maji, usafirishaji, na miundombinu ya barabara.
Kazi zote zimefanyika kutekeleza ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ahadi za Rais Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 pamoja na ahadi au mahitaji mengine yanayotokea katika ziara mbalimbali za viongozi.
Kwa mkoa wa Mwanza, kazi nyingi na kubwa zimefanyika kuhakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu kwa wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela anasema mikakati hiyo ya maendeleo inahusisha mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya na kushiriki shughuli za uzalishaji mali kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa.
“Tunapozungumzia Tanzania yenye uchumi wa kati kupitia maendeleo ya sekta ya viwanda ifikapo 2015, tunalenga kumwezesha kila Mtanzania pale alipo kuzalisha, kuuza na kufanya biashara kulingana na mahitaji, mazingira na mtaji wake,” anasema Mongella
Sekta za kilimo, uvuvi, uwekezaji na biashara ni kati ya maeneo muhimu yanayotumiwa na wakazi wa mkoa wa Mwanza kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotekelezwa na wakazi wa mkoa huo umewezesha mkoa wa Mwanza kushuhudia ukuaji wa uchumi kwa kwa asilimia 8 huku pato la mkoa likiongezeka kila mwaka.
Mongella anasema kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Pato la Mkoa wa Mwanza limeongezeka kutoka Sh10.05 trilioni mwaka 2016 hadi kufikia Sh11.3 trilioni mwaka 2017.
Kiwango hicho kimeufanya mkoa wa Mwanza kushika nafasi ya pili baada ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkoa pia umeshika nafasi ya pili Kitaifa kwa kuchangia asilimia 9.79 ya pato la Taifa mwaka 2017 kulinganisha na asilimia 9.69 ya mwaka 2016.
“Wastani wa kipato kwa mwaka kwa kila mwananchi umeongezeka kutoka Sh2.2 milioni mwaka 2016 hadi kufikia Sh2.3 milioni mwaka 2017.
“Ongezeko la kipato inaimarisha uwezo wa wananchi wa kununua na kuuza; hii inatoa ishara njema kwa uchumi wa mkoa na mtu mmoja mmoja,” anasema Mhe.Mongella.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.