Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Januari 29, 2025 amefungua rasmi Mkutano wa Mwaka wa Mameneja wa Makao Makuu na Kanda wa Benki ya NMB, uliofanyika katika Ukumbi wa Malaika jijini Mwanza, na kusisitiza kuwa mafanikio ya taasisi za kifedha yanapaswa kuanza na ustawi wa wafanyakazi wake.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Mtanda amesema ili benki iweze kufikia malengo yake makubwa ya kibiashara na kijamii ni lazima ijenge mahusiano imara kati ya menejimenti na watumishi wa ngazi zote.

Aidha, ameipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kutekeleza wajibu wake kwa jamii (CSR), akibainisha kuwa zaidi ya shilingi milioni 300 zilitolewa kusaidia jamii, ambapo zaidi ya shilingi milioni 60 zilitumika kuwasaidia wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Kanda Bugando.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mtanda amezitaka taasisi za kifedha kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Mwanza, akieleza kuwa mkoa huo unachangia asilimia 7.2 ya Pato la Taifa, ukiwa wa pili kitaifa baada ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ujenzi wa meli ya kisasa MV New Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 1,200, pamoja na uendelezaji wa reli ya SGR, utaifanya Mwanza kufikika kwa njia za anga, maji na reli na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.

Pia amesema Serikali imejenga Soko Kuu la Kisasa la Mjini Kati ili kuimarisha biashara za ndani na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje ya mkoa, hususan Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Amehakikishia Benki ya NMB kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono, huku akiwahamasisha wananchi kutumia huduma za benki hiyo kutokana na mtandao wake mpana na uaminifu wake kwa jamii.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Bw. Philbert Mponzi amesema benki hiyo imekuwa ikiandaa mkutano huo kila mwaka kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji wa mwaka uliopita na kuweka mikakati ya utekelezaji kwa mwaka unaoendelea.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.