Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhe. John Mongela amesema Serikali imeuweka mkoa huo kimkakati na uwekezaji kutokana na kuwa kitovu cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya uwepo wa shughuli mbalimbali ndani ya mkoa huo kwa wiki moja mfululizo,Mhe. Mongella alisema ili nchi ama mkoa wowote uweze kujulikana kimataifa ni lazima kuwepo na matukio yanayotambulisha kiuchumi,kijamii na kiutalii.
Alisema kuazia Oktoba 25 hadi Septemba Mosi, mwaka huu kutakuwa na shughuli ama matukio mbalimbali yakiwamo matamasha, warsha, mikutano ya kitaifa na kimataifa ndani ya mkoa ambayo itasaidia kukuza uchumi na kuibua fursa na maendeleo ndani ya jamii.
Alisema Mwanza ni miongoni mwa mikoa michache nchini ambayo Serikali imeiweka kimkakati wa maendeleo na uwekezaji kutokana na kuwa kitovu cha EAC hivyo kufanyika shughuli mbalimbali mkoani humo zitasaidia kukuza uchumi wa mkoa sambamba na jamii wakiwamo wafanyabiashara kufaidika.
“Leo tutaanza kuadhimisha siku ya fimbo nyeupe ambayo inawahusu watu wasioona ambapo wanawaomba wana Mwanza tuungane pamoja kuona namna kutatua changamoto zinazowakabili na hata kuthibiti vyanzo vinavyosababisha hali hiyo.
“Pia Oktoba 27 ,mwaka huu mkoa wa Mwanza utakuwa na tamasha la Tigo fiesta na siku inayofuata tutakuwa na mashindano ya Rockycity Marathon ambayo yatahusisha mbio za kilomita kuanzia tano hadi 42 ambapo nchi mbalimbali zitashiriki.
“Vile vile Oktoba 29-30, mwaka huu kutakuwa na kongamamo la ndege zisizo na rubani ambapo shughuli hii itakuwa ya kimataifa, kama mnavyojua teknolojia imekuwa sasa ndege hizo zitakuwa zinatumwa kwenda maeneo mengine na kutoa huduma kwa jamii, mbali na matukio hayo siku zinazofuata tutakuwa na shughuli ya maadhimisho ya siku ya Mwalimu yatakayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na kitaifa yatafanyika Mwanza,”alisema.
Mongela alisema faida za kijamii na kiuchumi zitakazopatikana kwa matukio hayo ni kujenga ushirikiano ndani ya jamii, vijana kupata fursa za kuonyesha vipaji vyao, wafanyabiashara wa hoteli kupata wateja.
Hata hivyo aliongeza kuwa katika matukio hayo, Serikali mkoani humo imejipanga kutumia fursa hiyo kuwaelezea namna Mwanza ilivyo na mazingira salama na rahisi kuzifikia hifadhi za taifa ikiwamo Serengeti.
Aliwataka wadau mbalimbali wanaohitaji uwekezaji ndani ya Mkoa wa Mwanza kujitokeza na kupewa ushirikiano na Serikali ili lengo la kimkakati liweze kutimia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.