Timu ya watumishi wa Serikali (RAS Mwanza) imeshindwa kutamba mbele ya timu ya Bakwata Mwanza baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1.
Timu hizo zilipimana vikali kwenye mchezo maalumu wa sherehe za Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W uliofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini humu.
RAS Mwanza wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe.John Mongella, waliliandama lango la Bakwata na kupoteza nafasi nyingi za awali.
Bakwata walitangulia kupata bao la kuungoza kabla ya RAS kusawazisha kwenye mchezo huo uliohudhuriwa na watumishi kwa ujumla,waumini wa dini ya kiislamu na wananchi wa madhehebu mbalimbali .
Ramadhan Khamis aliifungiau Bakwata bao dakika ya 30 baada kuwatoka walinzi wa RAS na kuachia kombora kali lililomshinda kipa Michael Ligola na kujaa wavuni.
RAS walipata pigo kwenye dakika ya 35 baada ya mshambuliaji wao John Mongela kuumia na nafasi yake ikachukuliwa na Gwandise Kalekele.
Hadi mapumziko Bakwata walikuwa mbele kwa goli 1-0 ambapo kipindi cha pili RAS waliingia kwa kasi na kulisakama lango la Bakwata kusaka bao la kusawazisha.Jitihada zao zilizaa matunda baada ya Said Mwalimubora kusawazisha akiwazidi walinzi wa Bakwata na kuuweka mpira wavuni dakika ya 70 ya mchezo.
Timu zote zilifanya mabadiliko, mabadiliko yaliyoinufaisha Bakwata kwa kuandika bao la pili kupitia kwa Hussein Bunyonyi baada ya kuwachambua walinzi wa RAS Mwanza kunako dakika ya 79. Licha ya RAS kusaka bao la kusawazisha wakiongozwa na Katibu Tawala Christopher Kadio, ukuta wa Bakwata ulikuwa imara na kuondosha hatari zilizoelekezwa langoni kwao na hadi mwisho wa mchezo huo Bakwata 2-1 RAS.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.