MELI YA MV. MWANZA YAPOKEA SHEHENA ZA SAMANI
Leo Machi 24, 2025 Mkuu wa Wilaya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameongoza hafla fupi ya mapokezi ya magari tisa yaliyobeba makasha yenye mzigo wa samani zitakazofungwa kwenye Meli ya Mv. Mwanza inayojengwa katika ziwa Viktoria.
Akizungumza katika mapokezi hayo Mhe. Makilagi amesema kuwasili kwa samani hizo ni hatua muhimu katika kuelekea kukamilisha mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji wake na ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2025.
“Hatua hii ya mwisho ni kielelezo tosha ya namna Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyoufungua Mkoa wa Mwanza, unao changia pato la Taifa kwa asilimia 7.2”. Mhe. Makilagi.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameitaka Menejimenti ya Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kuhakikisha inasimamia vema mradi huo ili ukamilike kama ulivyopangwa na kufanikisha azma ya Serikali ya kuboresha huduma ya usafiri kwa njia ya maji kwa abiria na mizigo kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa.
“Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuongeza chachu kwa ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na nchi jirani kwa kutoa huduma za usafiri zilizo salama, bora na za uhakika”. Amesema Mhe. Makilagi
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa TASHICO Bi. Amina Mtibampema amesema leo wamepokea vifaa yaani viti vya madaraja yote ambapo mara baada ya kukamilika kwa zoezi la umaliziaji wa meli hiyo kampuni hiyo ya meli itakwenda kufungua uchumi wa Mkoa, wafanyakazi wa TASHICO pamoja na Taifa kiujumla.
“Tutaendelea kusimamia mradi huu kwa maendeleo ya Taifa, na baada ya kupokea Vifaa hivi ufungaji utaanza mara moja”. Bi. Amina.
Mradi huo wa Meli ya Mv. Mwanza kwa sasa umefika asilimia 96 na fedha zilizolipwa hadi sasa ni asilimia 93. Aidha Meli hiyo itakapokamilika itakuwa ndiyo meli kubwa kuliko zote katika Ziwa Viktoria ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa 3.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.