MHE. MAJALIWA ATAKA SEKTA MTAMBUKA KUWEKA MSINGI MATHUBUTI KUIMARISHA LISHE NCHINI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) amezitaka sekta mtambuka kushirikiana katika kutekeleza afua za lishe ili kuondoa tatizo la utapiamlo, udumavu na ukondefu nchini.
Mhe. Majaliwa amesema ni lazima wizara za kisekta kama za Elimu, TAMISEMI, Kilimo, Uvuvi, Maendeleo ya jamii na Afya kushirikiana na wadau katika kuweka mikakati na mipango itakayosaidia kutekeleza sera na msingi mathubuti wa lishe nchini.
Mhe. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Alhamisi Oktoba 04
., 2024 katika Mkutano Mkuu wa kumi wa wadau wa lishe uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Malaika beach resort Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutokomeza aina zote za utapiamlo nchini ikiwemo kutekeleza mkakati wa kuimarisha lishe bora, kuajiri wataalamu wa lishe na kusaini mikataba na viongozi wa Mikoa na Wilaya ya kutekeleza afua za lishe.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Mkoa huo unaendelea kutekeleza afua za lishe na mikakati yote ya kuweka jamii kwenye afya bora na kuwatoa wananchi kwenye utapiamlo, unyongefu na udumavu wa akili na mwili.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwaalika wadau kwenye maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa kitakachofanyika Oktoba 14, 2024 kwenye uwanja wa CCM Kirumba ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Jimmy Yonazi amesema mkutano huo umeweka maazimio kadhaa yakiwemo ombi kwa Serikali kujumuisha masuala ya Lishe kwenye dira ya Taifa 2050, kuratibu na kuteleza masuala ya lishe kwa kipaumbele pamoja na kuimarisha sekta binafsi ili zishiriki kwenye masuala ya lishe.
Mkutano huo wa siku mbili umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo; "Kuchagiza mchango wa wadau wa kisekta ili kudumisha matokeo bora ya hali ya lishe nchini Tanzania".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.