Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amefika eneo la mtaa wa Mwinuko Manispaa ya Ilemela lenye mgogoro kati ya mzee Nyamonge Magabe na Bismak ambaye ajulikanaye kama AL-RAHBY na kuagiza kusitisha kwa shughuli zote za uendelezaji wa eneo hilo na matumizi ya aina yoyote ikiwa ni pamoja na ukataji wa kuni hadi tarehe 15/12 mwaka huu yatakapotolewa maamuzi kuhusiana na eneo hilo.
Mkuu wa Mkoa amefika eneo hilo akiwa na wataalam wa Ardhi wa Mkoa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo ambapo mzee Magabe amekuwa akilalamika kutishiwa na kutaka kunyang'anywa eneo kwa njia za kitapeli na udanganyifu kwa kuonyesha kuwa hakuwahi kuwepo hapo wakati yeye akidai kumiliki eneo hilo tangu mwaka 1987 likiwa bado pori, ameongeza kuwa amefungua kesi kadhaa dhidi ya watu mbalimbali waliokuwa na nia ya kumpora eneo hilo.
Awali tarehe 03/11/2017 Mhe. Mkuu wa Mkoa aliwaita watumishi wote wa Idara ya Mipango Miji na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya upimaji wa eneo la Mzee Magabe lililopo mtaa wa Mwinuko.
Mzee Magabe alieleza mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa shamba lake lina ukubwa wa ekari mbili na amekuwepo hapo tangu mwaka 1987 wakati taarifa iliyowasilishwa na Idara ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inaonyesha eneo hilo limo ndani ya viwanja namba 658,659 na 661 villivyopimwa na kumilikishwa kwa AL-RAHBY.
Kutokana na mkanganyiko huo Mhe. Mongella aliwataka maofisa hao wa Ardhi kupitia tena mipaka ya eneo la Mzee Magabe na kufanya uthamini na uchunguzi wa kina wa mgogoro huo na taarifa hiyo kuwasilishwa kwake si zaidi ya tarehe 13/11/2017 na tarehe 14/11/2017 Mhe. Mkuu wa Mkoa amefika eneo la mgogoro kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.