Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella ametumia fursa ya uzinduzi wa Mwongozo wa uwekezaji kuwakaribisha watu wote na makampuni kuja kuwekeza Mwanza, na kuwahakikishia huduma bora wakati wowote kutoka Ofisi ya Mkoa wa Mwanza ili kuufanya uwekezaji kuwa wa tija na wenye kukua kwa maslahi ya Nchi na Watanzania kwa ujumla.
Mhe. Mongella ameongeza kuwa,Mwongozo unadhamiria kukuza uwezo wa ushindani wa Mkoa wa Mwanza katika maeneo ambayo Mkoa una fursa za kiuchumi na kukuza uwezo wa uzalishaji katika sekta muhimu za msingi ili kuleta maendeleo endelevu yatakayochangia kukua kwa pato la jumla la Taifa na ustawi wa mkoa wa Mwanza.
Mongella ameongeza kuwa Mkoa wa Mwanza na Wilaya zake wamedhamiria kutoa kipaumbele katika uwekezaji na kutoa huduma stahiki na motisha za kuvutia wawekezaji katika Mkoa.
Aidha, Serikali ya Mkoa wa Mwanza na mamlaka zake za Serikali za Mitaa zimeandaa mipango mwafaka na mazingira bora ya uendeshaji na ya kibiashara na watakuwa wanapatikana wakati wote ili kutoa maelezo zaidi kuhusu fursa zilizopo kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza.
Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa wa Mwanza umeandaliwa sambamba na Sera ya Uwekezaji ya Tanzania pia unaainisha fursa za uwekezaji zinazopatikana katika mkoa na unaendana na dira ya mkoa wa Mwanza na umeandaliwa kulingana na mifumo ya kimaendeleo ya kitaifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016-2021.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.