MICHUANO YA SHIMIWI,RAS MWANZA YAFUNGUA DIMBA KWA USHINDI
Timu ya RAS Mwanza ya mpira wa pete imefungua Dimba kwa ushindi wa magoli 27-4 dhidi ya Bodi ya Pamba michuano ya michezo ya wizara na idara za Serikali,SHIMIWI inayoendelea kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Mwiba mkali katika mchezo huo alikuwa ni mchezaji Winfrida Martin kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira,MWAUWASA aliyepachika magoli 26 na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao muda wote wa mchezo na kuwalaza na viatu mara baada ya mchezo huo.
Msimamizi wa mazoezi wa timu hiyo Veronica Mponzi amebainisha licha ya muda mchache wa maandalizi lakini anajivunia ubora wa wachezaji wake na wenye uzoefu na michuano hiyo.
Hata hivyo katika mchezo wa pili dhidi ya Haki za binadamu timu hiyo kutoka Mwanza ilifungwa kwa mbinde magoli 22-17 kabla ya jana kutambiwa na timu ya Bunge Sports magoli 54-10
"Huu ni mchezo wa pili tumepoteza, wapinzani wetu walitumia vizuri nafasi walizopata,tumejipanga vizuri kuhakikisha mchezo unaofuata dhidi ya Wizara ya Elimu tunawafanyia Ubaya Ubwela na kutoka na ushindi mzito",amejinasibu Mponzi
Kiongozi wa msafara wa timu ya RAS Mwanza ambaye pia ni beki katili mstaafu, Denis Kashaija amebainisha wachezaji wote wapo vizuri na timu ya wanaume kwa upande wa mchezo wa riadha itashuka kufukuzana na upepo Septemba 26 mbio za mitaa 400
Timu hiyo kutoka Mwanza inashiriki michezo ya mpira wa pete,riadha,vishale,draft pamoja na michezo ya jadi karata na bao na imeanza Septemba 18,2024. na itahitimishwa Oktoba 5,2024
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.