Katika kutekeleza mikakati ya kimaendeleo inayofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Halmashauri ya wilaya ya Buchosa iliyopo mkoani Mwanza ni mojawapo ya halmashauri iliyojipanga katika kutekeleza mikakati hiyo.
Hayo yameelezwa hii leo katika kikao cha 4 cha baraza la madiwani kilichofanyika Wilayani humo kilichoongozwa na mwenyekiti Idama Kabanzi diwani wa kata ya Nyanzeba na kuhudhuriwa na madiwani, Wajumbe pamoja na mbunge na viongozi mbalimbali wa halmashauri hiyo huku lengo likiwa ni kujadili ajenda mbalimbali za kutekeleza mikakati ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, kwa upande wa sekta ya afya mbunge wa halmashauri ya wilaya ya Buchosa Dkt. Charles Tizeba ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuweza kujenga hospitali ya kisasa wilayani hapo ambayo inatarajia kuanza kutoa huduma ifikapo mwishoni mwa mwaka huu ambapo walengwa wakuu watakuwa akina mama wajawazito, watoto pamoja na wananchi wote wa halmashauri ya wilaya ya Buchosa.
"Nipende kuishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kutujengea hospitali hii ya kisasa ambayo inatarajia kuanza kutoa huduma ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. " Alisema Tizeba.
Naye, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Buchosa, Bw. Chrispine Luhanda ameeleza kuwa hospitali hiyo itakapokamilika wananchi wa Buchosa ambao wengi wanakwenda kupata huduma ya afya sengerema na geita ambapo wanatembea umbali mrefu watakuwa wamesogezewa huduma hiyo kwa ukaribu zaidi.
"Matarajio yetu ni kwamba baada ya hospitali hii kukamilika wananchi wa halmashauri ya Buchosa watakuwa wamesogezewa huduma hii ya afya kwa ukaribu, sababu wamekuwa wakienda kupata huduma hiyo sengerema, geita na wengine kuvuka hadi Mwanza. "Alisema Luhanda.
Aidha, diwani wa viti maalumu halmashauri ya wilaya Buchosa, tarafa ya ya Nyehunge Ndg. Mwamini Antony Gandama ameshauri viongozi hao kuweza kutembelea miradi wanayoisimamia ili kuleta tija na matokeo ya pesa zinazotolewa na serikali yaonekane kwa wananchi wa halmashauri hiyo.
" Nipende kuwashauri viongozi kuweza kutembelea miradi wanayoisimamia ili ilete tija na matokeo ya pesa zinazotolewa na serikali yaweze kuonekana kwa wananchi wa Buchosa. " Alisema Gandama.
Katika hatua nyingine Eng. Kassian Mwitike, Meneja wa usambazaji maji sengerema amebainisha kuwa wameshaweka mikakati mbalimbali kwa kushirikiana serikali na kupitia vyanzo mbalimbali kukamilisha mradi wa maji wa Nyakalilo na Bukokwa ulioanza mwaka 2014 ambao umeshafikia asilimia 90% ya utekelezaji wake na kusema utakamilika ifikapo mwezi disemba mwaka huu ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.
"Kwa mikakati tuliyojipanga kupitia wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini, serikali na kupitia vyanzo mbalimbali tumejipanga kuhakikisha mradi wa maji wa Nyakalilo na Bukokwa ambao umeshafikia asilimia 90% ya utekelezaji wake kukamilika ifikapo mwezi disemba. " Alisema Mwitike.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kikao hicho Idama Kabanzi amewaomba wakurugenzi na viongozi wote kuhakikisha wanakaa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili halmashauri ya Buchosa ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na changamoto hizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.