Zaidi ya wananchi laki moja wilayani Magu Mkoani Mwanza wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria uliojengwa na Serikali kwa gharama ya Sh.bilioni 16, ukitarajiwa kuzifikia baadhi ya wilaya za Mkoa huo ikiwemo wilaya ya Misungwi.
Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya kituo cha usambazaji maji kilichopo kitongoji cha Busulwa wilayani Magu kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Philemon Sengati alisema changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Magu ni ukosefu wa maji safi na salama ya uhakika japo kuwa wapo mita chache kutoka ziwa Victoria.
Alisema kukamilika kwa mradi huo mwezi Septemba mwaka jana umekuwa mkombozi kwa wananchi ambapo hali ya upatikanaji wa maji kwa wilaya hiyo ni zaidi ya asilimia 80 ,huku upatikanaji wa maji kwa eneo lengwa ambalo ni Magu mjini likiwa ni zaidi ya asilimia 100 ambapo uzalishaji huo unauwezo wa kuzalisha maji lita za ujazo million 7 zenye uwezo wa kukudhi mahitaji ya watu zaidi ya laki moja.
“Pia tunayo miradi mingine katika maeneo mbalimbali ya pembezoni ambayo inaendelea huku mingine ikiwa imekamilika mfano kata ya Lugeye, Nsolwa bubinza na Kitongosima ambayo yote imefadhiliwa na serikali yenye lengo la kuwaondolea wananchi changamoto zilizokuwa zikiwakabili”alisema Sengati.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa wa Mwanza Salum Kalli amewataka watendaji wa serikali wawe waaminifu na watekeleze miradi ya serikali kwa viwango vilivyo bora na kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma pasipo kuhujumu miundombinu mbalimbali inayotekelezwa.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe.Dkt. Severine Lalika alisema Mradi huo wa maji ukitumika vizuri kwa wakazi wa Magu pato lake litakuza uchumi wa wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
Paulo Shabani na Samson Gibui Wakazi wa kijiji cha Busulwa waliipongeza serikali kuwajenge mradi huo ambao umeweza kuwaepusha na magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakiwatesa kipindi cha nyuma kutokana na kutokutumia maji yasiyokuwa safi na salama .
“ Tulikuwa tukitumia maji ya ziwani tena bila kuchemshwa hivyo tulipata magonjwa ya mlipuko kama magonjwa ya tumbo (Typhoid), lakini kwa sasa tunapata maji yaliyo safi na salama tena yenye dawa” alisema Gibui.
Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mwanza walifanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambapo wameweza kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ikiwemo ujenzi wa jengo la kuhifadhi mizigo, jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege, urefushaji wa barababara ya kuruka na kutua ndege kwa mita 500, kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko vipya vitakavyokuwa vinafanya kazi katika maeneo ya Kayenze, Bezi ,Chato,Nkome ,Bugorola na Ukara.
Pia waliendelea na ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa chelezo, ujenzi wa meli mpya ndani ya ziwa Victoria ,ukarabati wa meli za Mv.Viktoria na Mv.Butiama , ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilometa 3.2 linalojengwa busisi na kigongo pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wilayani Magu unaosimamiwa na MWAUWASA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.