Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe.Juma Sweda ameyataka makundi yote ya kijamii Wilayani humo kushirikiana kupiga vita ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambao ni miongoni mwa vikwazo dhidi ya juhudi za Serikali za kupambana na umaskini nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya wiki nane ya kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana inayoendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Kivulini la jijini Mwanza kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo, amesema pesa wanazopata wanaume wa Wilayani humo kutokana na mavuno zinawalevya, matokeo yake ndoa zinavunjika, watoto wanashindwa kusoma na hali ya maisha inakuwa ngumu kwenye familia.
“Kaa na familia yako kipindi hiki cha mavuno mpange kitu gani cha maendeleo mnafanya, kwa ajili ya maendeleo yenu lakini pia kusomesha watoto wenu kwa kuwatimizia mahitaji na vifaa vya shukeni ili wawe nadhifu,”alisema Sweda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Eliud Mwaiteleke alisema, kampeni hiyo itahusisha Kata 27, Vijiji 113 na Vitongoji 724,ambapo walikubaliana kila kata ifanye uzinduzi kuweka msukumo kwa jamii wa kupinga ukatili kwa wanawake na wasichana na kukuza hali ya kujiletea maendeleo kwenye Kaya, kusomesha watoto na kupambana na mimba za utotoni.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Kimvulini Yassin Ally alisema, ni wakati sasa wa jamii kubadilika na kuondokana na imani potofu kwa kuzani kila maumivu ni kurogwa sambamba na kufuja pesa zitokanazo na mavuno kwa kutumia na wanawake wa nje badala ya kufanya maendeleo kwa kujenga nyumba nzuri na kusomesha watoto.
“Unalalia godoro Dodoma Ngumaru (godoro lililotengenezwa kwa majani yaliyokauka) ukiamka asubuhi shingo inakuuma, mgongo unauma halafu unasema nani kanikalia usiku unakimbilia kwa waganga wa kienyeji kwanini usinunue godoro zuri? Tubadilikeni ndugu zangu”alisema Ally.
Hata hivyo Wanawake na wanaume Wilayani humo walitumia kampeni hiyo kusukumiana lawama kila upande ukiushutumu mwingine kusababisha vitendo hivyo vikiwemo mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa.
Fransico Kiyumbi alikuwa wa kwanza kuanza kurusha madongo dhidi ya wanawake akisema baadhi yao huwafanyia waume zao ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa kuwanyima chakula na unyumba kutokana na kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa.
Regina Kubunga alijibu mapigo kwa kutaja madhaifu ya wanaume ikiwemo baadhi yao kutotimiza wajibu wa kuhudumia familia kiasi cha wanawake kulazimika kutumia akili na mbinu mbadala kutafuta fedha za kugharamia chakula na mahitaji mengine ya familia ikiwemo elimu ya watoto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.