Mkoa wa Mwanza umefanikiwa kupanda miti zaidi ya 10,000,000 ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kutunza mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji na kutekeleza agizo la Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango aliyoitaka mikoa yote nchini kupanda miti ili kutunza mazingira.
Hayo yameelezwa leo Februari 22, 2023 jijini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima wakati akitoa taarifa ya utunzaji mazingira mbele ya Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Khamis Hamza Khamis ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani hapa.
Mhe. Malima amesema wameshirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) katika kufanikisha hilo huku mikakati ikiwa ni kupanda miti zaidi ya 50,000,000 ndani ya miaka mitano, ambapo miti hiyo imepandwa kwenye Taasisi ikiwamo shule.
“Tumewapa TFS (Wakala wa Misitu Tanzania) tenda ya kupanda miti hiyo na tumeanza kwenye shule tunaamini tutafanikiwa kwa sababu TFS wana utaalam wa kujua miti gani inayoweza kustawi katika maeneo yapi.
Kikubwa katika upandaji wa miti ni Changamoto inayotukabili ni uhaba wa maji ya kuimwagilia kwani miti mingi imepandwa maeneo ya vijijini,” amesema Mhe. Malima.
Akizungumzia kuhusu uchafuzi wa mazingira hususani nyumba za ibada na maeneo ya starehe katikati ya makazi ya watu, Mhe. Malima ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya ukaguzi kwenye maeneo hayo ili kujiridhisha kama vigezo vinazingatiwa.
“Piteni kwenye hayo maeneo yote mpite na ‘sound meter’ hatuwezi kupigiwa kelele hadi saa 7 usiku wakati kuna watoto na wagonjwa wanaohitaji kupumzika muda huo, Mwanza ni jiji kubwa tukitaka kulifanya livutie lazima tujiwekee taratibu,” ameagiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis amevitaka viwanda vyote nchini kutekeleza sera ya mazingira kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kutunza mazingira huku akivitaka kutenga fungu maalumu kusaidia shughuli zote za mazingira katika maeneo husika ikiwemo usafi, upandaji miti na kutoa elimu inayohusu mazingira.
“Tuachane na kutumia makaa ya miti tutumie teknolojia ya kisasa itakayotusaidia kulinda mazingira, wenye viwanda wahakikishe hawatiririshi maji machafu au yenye sumu kwenda kwenye makazi ya watu na kuleta athari kwa wananchi. Pia mhakikishe moshi hauleti kero kwa wananchi, tukigundua unafanya hivyo na kuwasabaishia athari za kiafya tutachukuliana hatua za kisheria,” amesema Naibu Waziri.
Katika ziara yake ya kikazi jijini Mwanza Naibu Waziri Khamis Hamza Khamis ametembelea mradi wa dampo la kisasa uliopo Kata ya Buhongwa na kiwanda cha Multi Cable LTD. kilichopo Kata ya Mhandu Wilaya ya Nyamagana kinachozalisha bidhaa za plastiki.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.