*Prof. Mbarawa mgeni rasmi kwenye hafla ya kusaini mkataba huo*
*RC Makalla asema Rais Samia anastahili pongezi ameweka hostoria kanda ya ziwa*
*RC Makalla asema usafirishaji minofu ya samaki, na utalii utakuzwa*
Leo Machi 28, 2024 historia imeandikwa kwenye Viwanja vya Jengo la mizigo (Cargo Terminal) la uwanja wa ndege wa Mwanza kwa kusainiwa rasmi mkataba wenye thamani ya Bilioni 29 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la kisasa la abiria katika uwanja wa ndege wa Mwanza.
Akiongea na wananchi, mgeni rasmi wa hafla hiyo Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB) Waziri wa Uchukuzi amesema Serikali imeendelea kuboresha viwanja mbalimbali vya ndege nchini na kwamba zaidi ya Shs. Trilioni 1.1 zimetumika na kwamba ana imani kubwa na Mamlaka ya viwanja vya ndege,TAA wanaosimamia kazi hizo.
Aidha, Prof. Mbarawa amewataka mamlaka hiyo kuwekeza kibiashara kwenye viwanja vya ndege ili miundombinu inayojengwa isaidie kuinua uchumi wa nchi na akatumia wasaa huo kubainisha kuwa uwanja wa ndege wa Bukoba uko salama na ndege zinatua na kuondoka wakati wote.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amemshukuru Rais Samia kwa kukubali pendekezo la kukabidhi ujenzi huo kwa Mamlaka ya Viwanja vya ndege ili liweze kukamilika kwa kasi na amempongeza kwa kuweka historia katika utekelezaji wa miradi kanda ya ziwa.
Aidha, amebainisha kuwa uwepo wa jengo hilo lenye uwezo wa kuchukua abiria 600 kwa wakati mmoja pamoja na upanuzi wa uwanja vitakuza utalii pamoja na kusaidia kusafirisha minofu ya samaki na mizigo mingine kutokea Mwanza moja kwa moja pamoja na kusaidia kukuza Utalii.
"Baada ya hili jengo kukamilika pamoja na miradi mingine inayojengwa Mkoani kwetu kama ule mradi wa SGR, Mwanza itakua na fursa kubwa sana kwa uwekezaji hivyo ni lazima wananchi tujiandae na neema hizo." Mhe. Michael Masanja, Mwenyekiti CCM Mkoa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Musa Mbura amebainisha kuwa kuanzia mwaka 2020 serikali imeendelea kufanya maboresho ya uwanja huo ikiwemo upanuzi wa barabara ya kutua na kupaa, ujenzi wa jengo la mizigo, kituo cha taarifa za hali ya hewa pamoja na jengo na mifumo ya kuongozea ndege.
Ameongeza kuwa mwaka 2024/25 Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) itafanya maboresho ndani ya muda mfupi ikihusisha eneo la biashara, eneo la Maegesho, barabara ya kuingia na kutoka kwenye jengo hilo, barabara kiunganishi kwenda kwenye ndege na kwamba ndani ya miezi 10 litakamilika chini ya Mkandarasi mzawa Taifa Mining and Civil LTD.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.