Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana ameahidi upatikanaji wa wingi wa Ng'ombe bora watakaokidhi mahitaji ya Viwanda vya nyama kwa masoko ya nje na ndani.
Akizungumza kwa niaba yake kwenye Kiwanda cha Chobo Investment kilichopo nje kidogo ya Jiji la Mwanza wakati wa ziara iliyofanywa na uongozi kutoka Shirika la ndege nchini ATCL, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, Emil Kasagara amesema kupitia shamba la Serikali la Mifugo la Mabuki tayari kuna mpango maalum unaowashirikisha wafugaji namna ya unenepeshaji ng'ombe, elimu ambayo wataisimamia kuhakikisha inawafikia wafugaji wengi.
"Mkurugenzi Mtendaji Shirika letu la ndege mpango huu wa kunenepesha utakuwa unatoa ng'ombe 900 wenye ubora kila baada ya miezi mitatu, hali ambayo itawapa soko zuri la nyama hasa la nje ndugu zetu wenye viwanda." Amesisitiza Kasagara.
Amesema wanamshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea kwenye shamba la Mifugo ng'ombe 500 maalum wa nyama ambao hadi sasa wamefikia idadi ya 526 ambao wataongeza tija viwandani.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amebainisha kuwa lengo la ziara hiyo ni kujionea Uzalishaji wa nyama hizo, changamoto wanazopitia ili zifanyiwe kazi na mamlaka husika kabla ya ndege hiyo mpya ya mizigo haijaanza kufanya safari zake.
"Sisi kama ATCL tuna matumaini makubwa ya kufanya biashara na Mkoa wa Mwanza hasa ikizingatiwa wingi wa Mifugo ulipo ukanda huu pamoja na rasilimali ya Ziwa Victoria lenye samaki, la msingi ni kuwepo na mshikanano wa pamoja hasa kutoka Taasisi za Serikali kutowakwamisha hawa wafanyabiashara wa minofu, masoko ya nje hayataki ubabaishaji wa muda".Mhandisi Matindi
Mkurugunzi wa Kiwanda cha Chobo Investment,John Chobo amesema ujio wa hiyo mpya utakuwa mkombozi kwao kwani ndege ya awali iliyokuwa inawachukua na abiria haikuwa na tija kwao kwani ilikuwa inachukua mzigo mdogo
Ndege mpya ya mizigo ya ATCL inatarajia kuwasili nchini katikati ya mwezi huu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.