Wakati Watanzania wengi wakipoteza maisha, kupata majeraha na ulemavu wa kudumu kutokana na ajali za barabarani, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amesema wamejipanga kupunguza ajali hizo kwa kuchukua hatua na kuweka mikakati mbalimbali ikiwamo kuwahamasisha bodaboda kufuata alama na ishara zinazotolewa na wasimamizi wa sheria.
Mhe.Malima ameyasema hayo leo Machi 13, 2023 jijini Mwanza wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kitaifa inayofanyika mkoani hapa kuanzia Machi 14 hadi 17 huku Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa mgeni rasmi ambapo kauli mbiu ni 'Tanzania bila ajali inawezekana - Timiza wajibu wako'.
Mhe.Malima amesema kwa kipindi cha Januari - Desemba, 2022 jumla ya ajali kubwa 81 zimeripotiwa, zilizosababisha vifo vya watu 71 na majeruhi 96, huku ajali za pikipiki pekee zikiwa 30 zilizosababisha vifo vya watu 25 na kujeruhi 26 ambapo ameeleza kwamba mwelekeo wa takwimu hizo siyo mzuri na kuwataka watumia barabara kuzingatia sheria ikiwamo kuacha mwendokasi, ulevi, kujaza abiria na mizigo kupita kiasi na ubovu wa vyombo vya moto.
Amewataka watumiaji wa barabara mkoani hapa kukagua vyombo vya moto mara kwa mara ili kuepusha ajali zinazotokana na ubovu wa vyombo hivyo, huku akisisitiza kutoegesha barabarani kwa zaidi ya saa mbili magari mabovu yaliyoharibika.
"Mwanza tuna kauli mbiu ya kudumu kuhusu usalama barabarani inayosema 'karibu mkoa wa Mwanza:- tafadhali zingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, epuka adhabu kali'," amesema Mhe. Malima.
Vile vile, Mhe. Malima amewataka abiria kutoshabikia vitendo vya ukiukwaji wa sheria ikiwamo mwendokasi bali wakemee na kutoa taarifa kwa jeshi la polisi wanapoona ukiukwaji huo.
"Wananchi walio kandokando ya barabara wasijichukulie sheria mkononi inapotokea ajali katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuepuka kuchoma matairi na kuweka magogo kwa nia ya kufunga barabara kwa sababu hali hiyo huleta usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara ambao wana matatizo mbalimbali," amesema Mhe. Malima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.