Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana ametoa wito kwa Wizara inayoshughulikia vijana kushirikiana na sekta mtambuka kama SIDO na TEMDO kuhakikisha wanaliingiza kundi hilo katika uzalishaji unaotumia teknolojia ya kisasa.

Ametoa wito huo mapema leo tarehe 17 Februari, 2026 ofisini kwake wakati alipowapokea na kuzungumza na ugeni kutoka Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana waliopo Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.

“Nyie kama Wizara mnaoshughulikia vijana muna wajibu wa kuhusisha sekta zingine ili kubaini kama kuna miundombinu, mitaji au teknolojia rahisi za kukuza ubunifu wao ili kuhakikisha makundi ya ujasiriamali wanajiajiri kwa kutumia fursa zilizopo na kuleta tija.” Ndugu Elikana.

Aidha, ametoa rai kwa wizara hiyo kuangalia namna ya kuwaingiza vijana kwenye ajira zisizo rasmi kwa kuwaingiza kwenye ufugaji, kilimo na viwanda kama vya kutengeneza vyakula vya mifugo na kukuzia vifaranga vya samaki ili kulitoa taifa kwenye changamoto ya ajira kwa vijana.

Bw. Edward Haule, Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini na mratibu wa mfuko wa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Maendeleo ya Vijana amesema Wizara imejipanga vema kuhakikisha kundi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa linapata ajira.

Ameongeza kuwa wizara inahakikisha kuwa vijana wanakuwa na shughuli endelevu zinazozalisha kipato na ajira kwa wengine na katika kufanikisha hayo Wizara itaandaa Mazingira wezeshi ya kimiundombinu na mitaji sambamba na kuhusisha taasisi binafsi.

Aidha, amewataka Vijana kuhamasika na kutumia fursa hiyo kwa kuanzisha Miradi yenye tija kulingana na rasilimali zinazopatikana kwenye Mazingira yao ili waweze kujumuishwa kwa urahisi kwenye programu za maendeleo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.