Watumishi wasio waadilifu wazidi kuididimiza Wilaya ya Ukerewe baada ya kubainika kuhusika na wizi wa fedha za mapato wakati wa ukusanyaji kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vinavyoingiza mapato.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho kilicho hudhuliwa na baadhi ya Madiwani, Wakuu wa idara, Kamati ya Ulinzi na Usalama na watumishi wa Halmashauri baada ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella katika visiwa 38 vya Wilaya hiyo alisema hali ya Wilaya hiyo haina unafuu wowote, kila alipopita wanasema wanalipa kodi lakini wakiulizwa fedha zilipo hazijulikani.
Alisema kuna wizi unaoendelea watu wanatumia visiwa kama fursa ya kuiba mapato hivyo hawataweza kuwaacha, wataanza na kufunga mianya yote ya ulaji, watendaji warudi kwenye mstari na wasikubali kudanganywa na vitu vidogo bali wasimamie haki na utaratibu na kuacha kuhujumu mapato kwa kuwa imebainishwa uwepo wa mapato mengi hadi sasa hayajaingizwa kwenye mfumo.
“Yeyote atakaye thibitika kuwa ni tatizo atang’oka mnaweza mkaishi kwa kuiba?..tunapita kwa wananchi tumekuta wamejenga madarasa, lakini Halmashauri haifanyi chochote hata kuezeka wameshindwa kodi mnakusanya lakini hata kuwarudia wananchi mkajenga vyoo hamna, kazi yenu ni kuchukua hela kila tunapopita wananchi wanaimba halmashauri..halmashauri yenyewe haionekani.”alisema Mongella.
Hivyo aliahidi kuanzisha mfumo wa kufanya ukaguzi kila wiki kwa kipindi cha miezi sita huku akipiga marufuku kutoa fedha zitokanazo na mapato nje ya mfumo wa serikali kwa sababu utumiaji wa mapato nje ya mfumo ni tatizo sugu kwa Wilaya hiyo na ndiko mapato yanapopotelea .
Mongella aliagiza wapange safu mpya ya ukusanyaji mapato itakayoshirikiana na timu itakayotoka Mkoani kuja kuunga nguvu na kuifanya mifumo yote irudi kwenye mstari pia aliwataka watumishi kujituma na kufanya kazi kwa moyo ili kuchochea maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Cornel Magembe alisema Rais aliweka dhamana ili kuhakikisha anaisimamia Wilaya hiyo, hivyo alimtaka Mkurugenzi kubadilika na kuwa mkali ili watumishi wamtambue yeye ni nani, inaumiza sana wakati mwingine mkurugenzi anaitisha kikao cha CMT watakaotokea ni watu wanne wengine watakuwa wanapita pembeni wala wasisikilize kinacho jadiliwa, asipobadilika miradi iliyopo itamshinda.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo hilo Joseph Mkundi alisema watumishi wasipoweza kujitambua na kujua wajibu wao ni upi kutaitajika nyenzo za ziada kufanya wawajibike kwenye nafasi zao ili kutimiza wajibu na kuitendea haki taasisi.
“Tuna fursa nyingi sijui tuna kwama wapi, lazima tujitoe mhanga na kuwa makini katika majukumu yetu” alisema Mkundi.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo George Nyamaha ameahidi kushirikiana na wataalamu ili kumaliza tatizo hilo na kuwataka watumishi kubadilika katika suala la ukusanyaji wa mapato na wasitangulize sana posho kuliko kujitolea kutenda kazi yenye kuleta tija na maendeleo.
“Hatukuwa na nia mbaya kwenye ili jambo lakini sijui hii changamoto itaweza tusaidia tukatoka kama inawezekana siku moja hawa watu wa makao makuu wakiondolewa hii sheria ya kuwa mtu akitoka lazima alipwe posho labda hapo tunaweza tukabanana vizuri mimi ninafanya kazi nyingi ya kujitolea hawa wenzangu wanamishahara lakini unaweza kumwambia mtu toka nenda na asiende kwa sababu hajalipwa posho ya kutoka”alisema Nyamaha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.