Wadau wa Maendeleo na Taasisi mbalimbali za maendeleo zimetoa vifaa mbalimbali vikiwemo meza, ndoo, sabuni, diaba na matenki ya maji kwa ajili ya kusaidia kwenye mapambano ya Corona.
Vifaa hivyo vimepokelewa jijini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella ambaye amezishukuru taasisi hizo na wadau hao wa maendeleo kwa moyo wa kujitoa katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye mapambano ya ugonjwa wa homa ya mapafu( Corona) ambalo kwa sasa ni janga la dunia.
Aidha Mhe.Mongella amewataka wadau hao wa maendeleo kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto kwa kuweka mazingira yao katika hali ya usafi, kwa kunawa mikono kwa maji na sabuni kwa kutmia vitakasa mikono.
“ Nawashukuru sana wadau kwa kutoa vifaa hivi na kwa baadhi ya maeneo mmeshiriki pia kutoa chakula, lakini pia niwashukuru sana viongozi wa dini mnafanya kazi kubwa sana, kwa mahubiri na mafundisho yenu juu ya hili janga la Covid -19,” alisema na kuwataka wadau wengine zaidi kujitokeza kwa ajili ya kutoa vifaa vingine zaidi.
Mhe.Mongella ameongeza kuwa ugonjwa wa Corona ambao unaenea kwa kasi hivi sasa duniani ni hatari sana kwa maisha ya binadamu na kuwataka wananchi na watalaam kutofanya uzembe wa aina yoyote kwenye mapambano ya Corona.
“ Niwaombe viongozi wa dini, mashirika na taasisi zote tuendelee kuelimisha na kuwahamasisha wananchi namna ya kuendelea kuchukua tahadhari,” alisema na kuwashukuru Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi watendaji, maafisa tarafa, madiwani na viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji kwa jinsi wanavyoendelea kujitoa katika kuwahamasisha wananchi namna bora ya kupambana na ugonjwa huo.
Akizungumza kwa niaba ya wadau waliokabidhi vifaa hivyo Mwakilishi kutoka Taasisi ya Hindu Nilesh Popat alisema wao wameamua kutoa vifaa hivyo ili kuunga juhudi za Serikali kwenye mapambano ya Corona.
“Mhe. Mkuu wa mkoa tumekuwa tukitembea mitaani bado tunaona mahitaji ni makubwa ya vifaa vinavyohitajika na ndiyo maana tumeamua kutoa vifaa hivi,” alisema Popat.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RMO) Dkt. Thomas Rutachuzibwa alizishukuru taasisi na wadau hao wa maendeleo kwa misaada ya vifaa hivyo ambayo itawawezesha wananchi kujikinga zaidi na maambukizi ya Corona.
Kwa upande wake Shehe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke aliwataka watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili awanusuru na janga hili la ugonjwa wa corona.
“ Tunawaombea pia hawa waliotoa misaada yao na tunataka watanzania waendelee kuchapa kazi huku wakijikinga na ugonjwa wa corona,” alisema.
Baadhi ya taasisi na mashirika yaliyotoa misaada hiyo ni taasisi ya Hindu Union Temple iliyotoa chupa 28 za 500 mls za sabuni za kunawia mikono, Nyanza Roads Network iliyotoa ndoo 100 za plastic za lita 20 zenye koki, Siri Guru Sigh Sabha ambao wametoa meza 10 za chuma, tenki 10 za lita 250 kila moja na viti 5-0 vya plastic.
Taasisi nyingine zilizokabidhi vifaa ni pamoja na Cocacola Company iliyotoa madumu 100 ya lita 20 kila moja na Henan Afro –Asia Geo Engineering Company iliyotoa barakoa 200, deto sabuni zenye ujazo wa lita moja nne, vitakasa mikono chupa 48 kila chupa ikiwa na mls 250.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.