MRADI WA MAJI BUTIMBA KUTATUA KERO YA MAJI KWA WANANCHI WA ILEMELA -MWANZA : RC MAKALLA
*Kutoa zaidi ya lita Milioni 48 kwa Siku, Mabomba ya Maji yasambazwa Ilemela*
*Abainisha kuwa chanzo cha awali chafanyiwa upanuzi kukidhi mahitaji ya Usambazaji*
*Aunda kikosi kazi kuhakiki waananchi wanaozunguka Uwanja wa ndege wanaopaswa kupisha*
*Awataka wananchi kuishi kwa amani wakati taratibu za kuhakiki na kufidia wanaopaswa kuondolewa zikifanywa*
*Awaagiza Ilemela kumlipa Bi. Rahel Mkoma sehemu ya fidia yake ya Milioni 22 ifikapo mwezi Novemba*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wananchi wa Ilemela kuwa watulivu wakati Serikali ikikamilisha ujenzi wa Miundombinu ya usambazaji maji kwenye maeneo yao kufuatia ukamilishaji wa mradi mkubwa wa chanzo cha maji Butimba unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku.
Mhe. Makalla ametoa hakikisho hilo mapema leo oktoba 17, 2023 wakati wa Mkutano wake wa kusikiliza kero za wananchi ambao umefanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwa zaidi ya Saa 8.
Makalla amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejenga mradi mkubwa wa chanzo cha maji cha Butimba ambao tayari umeshaanza kutoa maji kwa majaribio na kwamba wananchi wa Ilemela watakua wanufaika wakubwa wa mradi huo pamoja na maeneo mengine ya Jiji la Mwanza.
"Mradi wa maji Butimba ndio tegemeo katika kutatua tatizo la maji, nimekagua mradi huo na maji tayari yameanza kutoka na mabomba yameshasambazwa Ilemela kwa ajili kuwafikia wananchi wote hivyo msiwe na wasiwasi Serikali yenu inafanya jitihada na hivi karibuni tatizo hilo linakwisha" amesema.
Aidha, Mhe Makalla amefafanua kuwa katika jitihada za kuhakikisha wananchi wa Mwanza wanapata maji, Serikali imeleta fedha zingine kwa ajili ya kufanya marekebisho na upanuzi wa mradi wa sasa wa maji wa Kapripoint ili kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha kwa kusaidiana na mradi mpya unaokamilishwa kujengwa.
Kuhusu wananchi waliovamia eneo la upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, Mhe. Makalla amebainisha kuwa ameunda kikosi kazi kitakachofanya tathmini ili kubaini wangapi wanapaswa kupisha upanuzi wa uwanja huo kama hitaji la Serikali la kuufanya kuwa wa kimataifa lakini kwa sasa amewataka kuishi kwa amani na wasiondolewe na mtu.
"Lipo hitaji la kupanua uwanja wa ndege kuwa wa kimataifa na jana nimeunda kikosi kazi cha kufanya uhakikia ili kujiridhisha nani atoke na maendelezo yaliyofanyika yanagharimu kiasi gani naomba mtoe ushirikiano kwenye kamati hii na kusiwe na uendelezaji mpya kuanzia leo kwenye makazi hayo ila naomba muishi kwa amani kabisa msibabaishwe na mtu". Amefafanua Mhe. Makalla.
Akiwa katika zoezi la utatuzi wa kero za wananchi, Makalla ameiagiza halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kumlipa Bi. Rahel Mkoma Tshs. Milioni 22 ifikapo mwezi Novemba 2023 ikiwa ni sehemu ya fidia kufuatia kutwaliwa kwa ardhi yake mwaka 2016 ambapo halmashauri hiyo imejenga shule ya Sekondari Bujingwa na akawataka watendaji kufanya upimaji shirikishi ili kuepusha migogoro ya ardhi.
"Watendaji nawaonya, acheni tabia ya kudharau maagizo ya Mkuu wa Wilaya na kusema ni ya Kisiasa, sikubaliani nalo suala hilo maana mnasababisha migogoro kuzidi kuwa mikubwa." Amesema Mkuu wa Mkoa wakati akitatua kero ya ardhi iliyotokana na halmashauri kutoa Kibali cha ujenzi kwa wananchi pamoja na uwezo wa katazo la Mkuu wa wilaya hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.