Zaidi ya wananchi Elfu 17 kati ya elfu 58 kwenye Vijiji 8 Kisiwani Kome - Buchosa wanatarajia kunufaika na Mradi mkubwa wa Maji unaotekelezwa na Kampuni Kamba's Company Group chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa zaidi ya Bilioni 2.2
Hayo yamebainishwa leo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima wakati alipotembelea Mradi huo kwenye kijiji cha Lugata na kubaini kuwa Ujenzi wa Mradi huo uliofikia asilimia 70 ya ujenzi upo kwenye hatua za mwisho za utekelezaji na kwamba ifikapo Mei mwaka huu utaanza kutoa Maji.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Maji atahakikisha Mkandarasi analipwa fedha zilizobaki kwa wakati na kufuatilia hatua za kupata msamaha wa kodi kwa mujibu wa mkataba wa mkandarasi huyo ili kuvitoa vifaa vilivyokwama bandarini mara moja.
Baadae Mkuu wa Mkoa alikagua maendeleo ya taaluma kwenye shule ya Sekondari ya Lugata na kusikitishwa na matokeo mabaya ya ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne pamoja na uwepo wa Miundombinu rafiki ya madarasa na akaagiza kukamilishwa kwa Ujenzi wa mabweni ili kuwapunguzia umbali wa kutembea wanafunzi wanapofika na kutoka shuleni hapo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lugata, Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe. Erick Shigongo amesema ukamilishaji wa mradi huo utasaidia kuwaokoa akina mama wanaokamatwa na Mamba ziwani kwa kufuata Maji na kwamba suala la Magonjwa ya Tumbo kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama itakua historia.
"Nimesikitishwa sana na maendeleo ya watoto kwenye shule hii, hatutafikia ndoto ya mafanikio kwa kufelisha watoto na ninatoa changamoto kwa walimu kutimiza wajibu na Serikali ihakikishe inatuletea walimu wa kutosha ili ujenzi wa madarasa uende sambamba ufaulu mzuri wa watoto." Amesema Mhe. Mbunge akiwa katika shule ya Sekondari ya Lugata.
Akizungumzia mradi wa Maji, Kaimu Meneja wa RUWASA Buchosa Mhandisi Elisha Sembo amebainisha sababu za kuchelewa kwa mradi huo kwa Miezi 6 kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa kuwasili kwa vifaa kutokana na taratibu za msamaha wa Kodi kwa vifaa vilivyonunuliwa nje ya nchi.
Naye, Ndugu Yahya Yusuph Mwenyekiti wa Kampuni ya Kamba's Company Group anesema kuwa endapo malipo ya fedha zilizobaki yatafanyika kwa wakati na kupatiwa msamaha wa kodi kwa vifaa vilivyopo bandarini mradi huo utakamilika kufikia Mei 2023
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.