Ujenzi wa kivuko kipya cha MV MWANZA ulioahidiwa na Mhe.Dkt. John Magufuli Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania umekamilika na kinatarajiwa kuimarisha huduma za uchukuzi wa majini katika Ziwa Victoria eneo la Kigongo-Busisi Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika hafla ya kushusha kivuko hicho majini Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongela amesema kivuko cha MV MWANZA kitaanza kutoa huduma zake ndani ya muda wa wiki tatu ili kuondoa adha ya usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
Kivuko hicho ambacho ujenzi wake umetekelezwa na Kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard tayari kimeshushwa majini kwa ajili ya kufanyiwa majaribio ya mwisho kabla ya kuanza kutoa huduma zake.
Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme Nchini -TEMESA uliotoa zabuni ya ujenzi wa kivuko hicho umesema kuwa kukamilika kwake kutaimarisha huduma za uchukuzi katika kivuko cha Kigongo-Busisi Mkoani Mwanza.
Zoezi la kushusha kivuko cha MV MWANZA kwenye maji limeshuhudiwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mwanza, Anthony Diallo amesema ujenzi wa kivuko hicho ambao umegharimu Shilingi Billioni 8.9 ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
Kivuko kipya cha MV MWANZA kilianza kujengwa Septemba mwaka jana ambapo kina uwezo wa kubeba Tani 250 za mizigo yakiwemo magari 36 na abiria elfu moja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.