Taharuki iliyokuwa imetanda Jiji la Mwanza juu ya mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Mtakatifu Mary’s Apostos, Yela Cosmas (17) kutekwa na watu wasiojulika huku wakiwataka wazazi wake kutuma fedha haraka vinginevyo wangempeleka nchini Zambia amekamatwa na Jeshi la Polisi akiwa amejiteka.
Ujumbe wa kutekwa kwa mwanafunzi huyo ulianza kusambaa juzi kwenye mitandao ya kijamii kupitia namba mpya ya simu 0689447247 ikiwa ni masaa machache baada ya wazazi wake kumsindikiza na kumpandisha basi la Sheraton kwenda shuleni.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo alisema tukio hilo lilitokea juzi na baada ya taarifa hiyo kuwafikia walianza kazi ya kufuatilia kwa kutumia kikosi maalumu walifanikiwa kumpata mwanafunzi huyo Lamadi mkoani Simiyu akiwa amejiteka lengo ni kupata fedha kutoka kwa wazazi wake.
“Mwanafunzi huyu alisindikizwa na wazazi wake hadi kituo cha Buruzuga na kupandishwa basi la Sheraton linalofanya safari zake kati ya Mwanza-Geita lakini baadaye alishuka na kusajili namba mpya ya simu 0689447247 ambayo wazazi wake hawaijui, ujumbe ule uliwataka wazazi fedha bila kutaja kiasi ili mtoto aachiwe kwani ametekwa vinginevyo angepelekwa nchini Zambia.
“Jeshi la polisi lilifuatilia tukio hilo kwa ukaribu kwa kutumia kikosi maalum na kumtia nguvuni mwanafunzi huyo Lamadi mkoani Simiyu akiwa salama na tunamshikilia ili kufanya mahojiano na baadaye tutamfikisha mahakamani kwani kitendo alichokifanya ni kinyume na sheria za nchi, tunaomba wanafunzi wenye nia kama hiyo waache haraka sana,”alisema Murilo.
Wakati huo huo polisi inamshikilia Lazaro Isaack (32) Mkazi wa Machinjioni mkoani Mwanza kwa kosa la kughushi nyaraka mbalimbali za Serikali, wizi kwa njia ya mtandao, kutapeli watu kwa kisingizio cha kutopata ajira, kujifanya mtumishi wa Serikali.
Kamanda Murilo alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi akiwa na kitambulisho cha kazi kutoka Vodacom Cap View Ltd na baada ya kufanya upekuzi katika makazi yake alikutwa na nakala 34 za TIN kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mikoa ya Mwanza, Pwani, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kagera, Mtwara na Shinyanga.
Murilo alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na vifaa vingi zikiwamo fomu za Serikali ambazo ziliwafanya watu wengi kuamini ni mtumishi wa Serikali na kuwatepeli kirahisi kwa kumpatia pesa ambapo polisi inaendelea kuchunguiza mtandao huo ili kuwabaini wanaoshirikiana katika mtandao huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.