Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima amehitimisha mashindano ya 23 ya Michezo ya UMITASHUMTA Kitaifa yaliyofanyika Mkoa wa Mwanza akimuwakilisha Waziri wa Nchi 0fisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo ambapo Mkoa wa Mwanza kwa mara ya pili mfululizo umeshika nafasi ya kwanza kitaifa.
Awali akihutubia katika kufungwa kwa mashindano hayo Mhe.Adam Malima aliwashukuru wote waliofanikisha zoezi hilo hadi kufikia kilele juni 29 na kuwaasa waendelee kufanikisha michezo katika shule zote Nchini.
"Napenda kuchukua nafasi hii ya pekee kabisa kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa wa Mwanza kwa uongozi wake imara uliofanikisha mashindano haya kufanyika kwa amani na usalama katika muda wote ambao mashindano haya yamefanyika," alisema Malima.
Vile vile hakusita kumpongeza Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa zakikisha kufanikisha kuwepo kwa mashindano hayo ambayo ni fursa pekee kwa vijana hao, katika kuonyesha vipaji vyao.
Mhe. Malima aliwasisitiza wanamichezo na wadau mbalimbali wa michezo kuhakikisha wanaienzi kauli mbiu ya mwaka huu inayosema, "Michezo Sanaa na Taaluma ni Msingi wa Maendeleo ya Mwanafunzi katika Taifa letu.”
Katika mashindano hayo Mkoa wa Mwanza umeibuka kidedea na kuwa mshindi wa kwanza kwa ujumla huku Mkoa wa Ruvuma ukishika nafasi ya mwisho Kitaifa kwa mwaka huu,ambapo Mwanza imekuwa bingwa kwa ya pili mfululizo huku katika mchezo wa netiboli wakifanya vizuri zaidi.
Naye Mwalimu Rehema Maruzuku ambaye ndiye kocha wa netiboli aliuzungumzia Mkoa wa Mwanza kwa nafasi ya pekee.
"Kwa netiboli Mkoa wa Mwanza umeshika nafasi ya kwanza kwa miaka mitatu mfululizo na ninafikiri kombe hili ni la Mkoa huu moja kwa moja kwa sababu ukimiliki kombe hili kwa miaka mitatu mfululizo basi ni la kwako"alisema Maruzuku.
Kwa upande wake mwalimu Tibu kutoka Singida hakusita kutoa maoni yake juu ya uendeshwaji mzima wa mashindano hayo.
"Mashindano ya UMITASHUMTA yameendeshwa vizuri, sema kuna baadhi tu ya Mikoa bado hawajazingatia sana suala la umri kama tumeamua kuwachezesha tu watoto wa umri fulani basi tuwalete watoto sahihi katika umri uliopangwa,"alisisitiza Mwalimu Tibu.
Nao wanafunzi waliouwakikisha vyema Mkoa wa Mwanza hawakusita kueleza siri ya mafanikio yao iliyowawezesha kutwaa ubingwa huo ambayo ni nidhamu nzuri,kufuata maelekezo ya walimu wao na waliongeza kuwa wamejifunza vitu vingi sana huku michezo ikiwaongezea ujasiri wa kujiamini kama wana michezo, na kufanya wapate marafiki wapya na kusisitiza kuwa mwakani watafanya vizuri zaidi, ambapo mashindano hayo yatafanyika Jijini Dodoma mwakani 2019.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.