MWANZA INA MAZINGIRA MAZURI YA KUWEKEZA KWENYE VIWANDA NA BIASHARA : RC MAKALLA
*Abainisha kuwa Mkoa unaelimisha wananchi kujihusisha na Uvuvi wa kisasa*
*Asema Mkoa huo utaendelea kuimarika na kuchangia pato la Taifa*
*Asema kuwa miradi ya kimkakati itachochea biashara na kukuza uchumi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amebainisha kuwa Mkoa huo unaendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanya uwekezaji na biashara ili wananchi wajishughulishe na shughuli za kiuchumi na kuweza kuinua pato la mtu mmoja mmoja na Taifa.
Makalla ameyasema hayo mapema leo Novemba 24, 2023 wakati akizungumza na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyopo Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Makalla amesema Mkoa huo upo kwenye zoezi kubwa la kutoa elimu kwa vijana ili waweze kujihusisha na uvuvi wa kisasa hususani kwenye vizimba jambo ambalo linahakikisha rasilimali za ziwani zinalindwa kwa manufaa ya muda mrefu.
"Kwa kuzingatia uwepo wa ziwa victoria, Mkoa wa Mwanza tunatoa elimu kwa wananchi kufanya uvuvi wa kisasa ambao ni wa kwenye vizimba na tunahamasisha wavuvi kuachana na uvuvi haramu", amefafanua.
Aidha, amebainisha kuwa uwepo wa miradi ya kimkakati inayoendelea kujengwa kama reli ya kisasa (SGR), Meli ya Kisasa ya MV Mwanza pamoja na Daraja la Kigongo-Busisi itasaidia sana kukuza biashara na kuchochea uchumi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mhe. Deodatus Mwanyika amesema kuwa pamoja na kamati hiyo kusimamia fedha zinazopelekwa kwenye miradi inahamasisha pia uwekezaji kwenye viwanda ili kuongeza thamani ya malighafi.
Ndege ya mizigo ambayo Mhe. Rais ameinunua inaweza kuwa chachu ya kufufua viwanda kwani inatoa nafasi ya kusafirisha moja kwa moja malighafi kwenda viwandani kwa hiyo Serikali inahamasisha ufugaji, kilimo na biashara za kisasa ili kupata tija.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.