Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda leo Februari 16, 2026 amekutana ofisini kwake na Msanii wa Filamu nchini, John Elisha maarufu kwa jina la Hamadi wa kombolela ambaye anatokea mkoani Mwanza.

Msanii huyo amefika kwa lengo la kujitambulisha rasmi, kutoa salamu pamoja na kuwasilisha baadhi ya tuzo alizozishinda katika mwaka 2025, ikiwa ni ishara ya mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye tasnia ya filamu nchini.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Mtanda amempongeza John Elisha kwa juhudi, ubunifu na nidhamu katika kazi zake, akisema kuwa mafanikio yake ni fahari kwa Mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla.

“Tunajivunia sana kuona vijana wetu wakifanya vizuri na kulitangaza jina la Mwanza kitaifa na kimataifa,” amesema Mkuu wa Mkoa.

Mhe. Mtanda amemhakikishia msanii huyo pamoja na wasanii wote wanaotoka Mkoa wa Mwanza kuwa ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano na sapoti wakati wowote watakapohitaji msaada wa kiofisi au kimazingira katika kukuza vipaji vyao.

Aidha, amewataka wasanii kutosubiri hadi wakumbane na changamoto ndipo watafute msaada, bali wawe na utamaduni wa kufika ofisini kujadiliana, kushauriana na kujenga ushirikiano wa karibu na uongozi wa mkoa.

Sambamba na hayo, Mkuu wa Mkoa amepongeza tena John Elisha kwa kazi nzuri anayoifanya na kumtaka aendelee kuiwakilisha vyema Mwanza kupitia sanaa yake, huku akihamasisha wasanii wengine kuongeza juhudi, ubunifu na mshikamano.

Kwa upande wake, John Elisha ameshukuru kwa mapokezi na ushirikiano alioupata, akiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha anaitangaza vyema Mwanza kupitia filamu na kazi zake nyingine za kisanii.

Mkutano huo unaonekana kuwa chachu mpya kwa wasanii wa Mkoa wa Mwanza, ukiashiria mwanzo wa ushirikiano imara kati ya uongozi wa mkoa na wadau wa sanaa katika kukuza vipaji na kuimarisha tasnia ya filamu nchini.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.