Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella amewasainisha kiapo cha uwajibikaji wakuu wa wilaya zote za Mkoa huo juu ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga ambapo amewataka kila mmoja awajibike katika eneo lake na kutoa taarifa ya za utekelezaji.
Mhe.Mongella alisema kutokana na jitihada za Serikali za kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga, mwaka 2018 vifo hivyo vimepungua na kufikia 151 lakini kuanzia Januari mwaka huu tayari vifo 46 vitokanavyo na uzazi vimetokea ndani ya mkoa huo.
“Sababu zinazoelezwa kusababisha vifo hivyo ni kwamba shinikizo la damu, kifafa cha mimba, kuvuja damu nyingi lakini sababu zingine inadaiwa zinatokana na maamuzi katika familia husika, vile vile na sisi viongozi wa umma tunahusika katika maeneo fulani.
“Sasa mimi kama Mkuu wa Mkoa naamua niingia mikataba na wakuu wa wilaya zote za mkoa huu, mkataba huu pia utawahusu wakurugenzi,meya na wenyeviti wa halmashauri, viongozi hawa niliowataja itakuwa rahisi mimi kuwabana na ndio maana nataka waje hapa mbele waweke sahihi zao.
“Kila mmoja akitoka hapa aende awajibike katika eneo lake kwa kufuatilia maendeleo ya utoaji huduma katika vituo, zahanati na hospitali zao, pia ni muhimu wakashuke ngazi za chini kuanzia vitongoji hadi vijiji na kuwatambua wajawazito na maendeleo yao, ikitokea kifo katika eneo lako unapaswa kutoa sababu za msingi kilichosababisha,”alisema Mongella.
Mongella alisema kumekuwapo na tabia ya viongozi wengi wa Serikali kuzungumza wakiwa maofisini kitendo ambacho kimeshindwa kuwa na mafanikio chanja kwa jamii juu ya mikakati inayopangwa, hivyo ni wakati muafaka kwenda vijijini na kuzungumza moja kwa moja na wananchi.
Alisema licha ya Serikali kuboresha sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya, zahanati, hospitali sambamba na kuongeza bajeti lakini tunapaswa kujitafakari kinachosababisha vifo vya mama na watoto vinaendeleo kutokea, hivyo aliwataka wadau wote wa afya, vyombo vya habari, viongozi wa dini na waganga wa tiba asili kuungana na kuelimisha jamii kuwahi kwenye tiba sahihi.
Naye Mratibu wa Afya mama na mtoto Mkoa wa Mwanza, Cecilia Mrema kuna haja ya Serikali kuboresha magari ya kubebea wagonjwa mkoani humo kwani kati ya ambulesi 9 kati 25 zilizopo ndizo zilizo na vifaa vyote vya kutolea huduma wakati mgonjwa akipelekwa hospitali ya rufaa.
Alisema katika Mkoa wa Mwanza sababu nyingi za vifo hivyo ni upungufu wa damu, vifaa, baadhi ya watumishi wa sekta ya afya kutokuwa na uelewa zaidi kwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka, gari za wagonjwa kutokuwa na mafuta na vifaa vyote vya tiba.
Vile vile alisema wajawazito kutumia dawa za kienyeji, kifafa cha mimba ambapo aliwataka akinamama kuhudhuria katika vituo vya afya ili kupata tiba sahihi.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa alisema uzinduzi wa kampeni ya uwajibikaji katika kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi yenye kauli mbiu ya ‘Jiongeze Tuwavushe salama’ ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu alilolitoa Novemba mwaka jana kwa kuelekeza kila mkoa kuweka mikakati ya kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Alisema kutokana na agizo hilo, mkoa wa Mwanza umejipanga kupitia kampeni hiyo kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto ambapo aliwataka watoa huduma kuongeza kasi kwani Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika sekta ya afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.