Tanzania ni nchi ya tatu katika bara la Africa katika Kipimo cha Utayari wa Kutumia Ndege Zisizo na Rubani kutokana na kuongoza katika miradi ya majaribio pamoja na faida zake katika maendeleo ya viwanda na masoko. Mkoa wa Mwanza umekuwa kituo cha kijiografia cha shughuli hii na sasa umedhamiria kuwa kitovu cha ubunifu wa mnyororo wa ugavi kupitia Maonyesho mapya ya Ziwa Victoria ya Ndege Zisizokuwa na Rubani (LVC), mradi ulioanzishwa na mamlaka za mkoa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), John Snow, Inc. (JSI), na wabia wengine. Uzinduzi rasmi wa maonyesho ya Ziwa Victoria ulifanyika hoteli ya Malaika Beach resort, Mwanza, tarehe 12 Desemba 2017, kuanzia saa sita kamili mchana.
Mkoa wa Mwanza una wakazi takribani milioni 2.8 na ni mmoja wa mikoa yenye watu wengi zaidi nchini Tanzania; wakati ukanda wa Ziwa Victoria, ukijumuisha na visiwa vyake, una watu zaidi ya milioni 30. Baadhi ya changamoto kuu kwa wakazi wa mkoa huu ni pamoja na sura ya nchi yenye vilima vingi, makazi kutofikika kwa urahisi, pamoja na visiwa, na miundombinu ya usafiri ambayo haijaendelezwa.
Maonyesho ya Ziwa Victoria yatavileta pamoja viwanda vya kutengeneza roboti na Ndege Zisizo na Rubani, wataalamu wa afya na usafirishaji, serikali na wabunifu kuonyesha na kujifunza ni kitu gani kinawezekana ili kusaidia mkoa kushughulikia changamoto zake za kipekee wakati ukinufaika na fursa nyingi ulizo nazo.
“Hasa tunakabiliwa na vikwazo vya kupeleka madawa visiwani na tunauona mradi huu wa Ndege Zisizo na Rubani kama fursa kubwa ya kuja pamoja na wabia kuona ni kwa jinsi gani unaweza kutusaidia katika kutafuta ufumbuzi kwa changamoto hizo,” alisema John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Katika miaka michache iliyopita, Afrika ya Mashariki imeshuhudia kupanuka kwa soko la nyanja ya ndege zisizo na rubani (UAV), ikiibuka kama mtumiaji wa kwanza wa teknolojia ya UAV. Kampuni bunifu tayari zimesha wekeza katika kufanya majaribio ya huduma mpya, ikiwa pamoja na kupeleka damu katika hospitali nchini Rwanda, kupeleka madawa kwenye vituo visivyofikika kwa urahisi mkoani Mwanza, na bidhaa zinazoletwa moja kwa moja nyumbani katika mkoa wa Arusha.
“Kuwezesha ndege zisizo na rubani za kubeba mizigo kama njia mpya ya usafirishaji na ugavi ina uwezo mkubwa wa kutokomeza matatizo ya mnyororo wa ugavi, na kukuza utoaji huduma kwa haraka kwa wananchi,” anasema Edward Anderson, Mtaalamu Mwandamizi wa Kudhibiti Maafa na TEHAMA wa Benki ya Dunia.
"Maonyesho ya Ziwa Victoria yatatoa takwimu muhimu zitakazowezesha usambazaji wa madawa na vifaa, hususani katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi na pia kusaidia uchunguzi wa magonjwa ya milipuko," anasema Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Maonyesho ya ndege zisizo na rubani, yatakayofanyika kwa kipindi cha siku tatu mwezi Oktoba 2018, yatakuwa ya kwanza ya aina yake katika Afrika, na yataonyesha maendeleo katika mifumo ya ndege zisizo na rubani ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii zisizofikika kwa urahisi na maeneo ya vijijini. Shughuli hii itajumuisha kipengele cha changamoto ya teknolojia kilichobuniwa na wataalamu wa Kiafrika kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
"Tunakaribisha maonyesho ya Ziwa Victoria kwani pamoja na kuwezesha usambazaji wa madawa kwenye maeneo yasiyofikika kwa urahisi, yataweka msingi kwa sisi Tanzania kuwa na mazingira bora ya udhibiti wa matumizi ya ndege zisizo na rubani katika sekta nyingine muhimu kama vile udhibiti wa maafa na uchoraji ramani za ardhi," anasema Mheshimiwa Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
“UAV zinaweza kuleta mabadiliko kwa kuhakikisha upatikanaji wa madawa ya kuokoa maisha katika maeneo yasiyofikika, hivyo kuokoa maisha. Kwa watendaji wengi wa mnyororo wa ugavi wa afya, uamuzi hautakuwa iwapo watumie UAVs kabisa, bali jinsi ya kuzitumia kwa kuzingatia gharama ndani ya rasilimali za usafirishaji zilizojumuishwa na kuunganishwa. Maonyesho ya Kanda ya Ziwa yanatoa fursa ya kipekee kwa wadau wa ndani na wa kanda kusukuma maendeleo ya ufumbuzi ili kushughulikia changamoto zao mahususi” anasema Yasmin Chandani, Mkurugenzi wa Ugavi, Mradi wa John Snow, Inc.
Kwa kuwaleta pamoja viongozi wa fikra wa Afrika na timu kutoka duniani hadi Ziwa Victoria kuja kushindana kwenye matatizo halisi ya dunia, shughuli hii inalenga kuleta chachu kwenye sera ya viwanda na mkakati wa ubunifu, na kuunganisha uwekezaji wa kimataifa na ubunifu wa ndani. Uzoefu huu utashamirisha ajenda ya viwanda na dira 2025 ya Tanzania.
“Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limefanya kazi kwa miaka mingi kuona jinsi teknolojia mpya na zinazoibuka zinaweza kuwanufaisha watoto walio katika mazingira hatarishi duniani. Katika mazingira ya aina nyingi ambayo tunafanya kazi, miundombinu duni au inayokosekana ni kikwazo cha kusambaza vifaa muhimu, habari na muunganisho kwa wale walio katika mazingira hatarishi. Tunaona teknolojia kama za Ndege Zisizo Rubani (UAV) zikitusaidia kuruka vikwazo katika miundombinu iliyopo au inayokosekana katika kusambaza vifaa, habari na muunganisho kwa wale walio na mahitaji makubwa. Ni matarajio yetu kuainisha, kupitia Maonyesho haya na kazi nyingine tunazofanya nchini Malawi au Vanuatu, jinsi UAV zinavyoweza kutumika katika mazingira yetu ya programu,” anasema Chris Fabian, Mshauri Mkuu, Ofisi ya Ubunifu ya UNICEF, New York.
Kwa maelezo zaidi kuhusu LVC 2018 tembelea tovuti hii:
https://www.lakevictoriachallenge.com/
Mawasiliano:
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
S.L.P. 119, Mwanza.
Simu: 028 2501037/2500366
Nukushi : 2501057 /2502114
Tovuti : http://www.mwanza.go.tz
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.