MWANZA WAJA NA MIKAKATI YA KUPAMBANA NA MAUAJI YA ALBINO
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Usimamizi wa rasilimali watu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Ndugu Daniel Machunda amesema watakaobainika kujihusisha na vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
Amesema hayo mapema leo Julai 15, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wakati akifungua kongamano la kupinga mauaji ya watu walio kwenye kundi hilo ambayo kwa siku za usoni yameibuka na kuhatarisha usalama wao katika maeneo mbalimbali.
Ndugu Machunda amefafanua kuwa mikakati mbalimbali imewekwa na Serikali ya mkoa kuanzia kwenye ngazi za vitongoji yanayolenga mapambano dhidi ya makundi kama vikongwe na wenye Ualbino ili kuhakikisha kila mwananchi anapata ustawi wake binafsi na jamii kwa ujumla.
Akitoa salamu za Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza, mratibu mwandamizi wa Jeshi la Polisi Denis Kunyanja amesema wanayo furaha kuwa sehemu ya mdahalo huo kwani wao wana jukumu la moja kwa moja la kuwalinda watu wenye Ualbino.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mwanza Edwin Soko amesema vyombo vya Habari mkoani humo kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino wanalaani vikali mauaji hayo kwani kundi hilo lina haki ya kuishi kama binadamu mwingine yeyote.
Aidha, ameliomba jeshi la Polisi kuendelea na kazi nzuri ya kulinda haki ya kuishi ya watu wote nchini wakiwemo wenye ualbino na kwamba wanaitendea haki ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa haki ya kuishi kwa kila mmoja.
Vilevile, ameahidi kuwa kwa kupitia vyombo vya habari wataendelea kuandika habari zenye suluhisho katika kulinda haki ya kuishi kwa albino na kwamba Mkoa wa Mwanza unaendelea kuwa kidedea kwenye habari zenye tija kwa kuhabarisha umma juu ya haki ya kuishi kwa makundi yote .
Akitoa risala ya Chama cha watu wenye Ualbino Mkoani humo Mashaka Enos amesema kuanzia 2006 hadi 2024 kumekua na mauaji yaliyokithiri ya watu wenye ualbino na siku za nyuma mkoa huo ulikua kinara kwenye mauaji ya watu wenye ualbino ambapo watu zaidi ya 20 wameuawa.
"Watu wenye ualbino wamekua wakikumbwa na manyanyaso na ukatili wa hadi kuuawa kutokana na imani mbalimbali, na wanateswa na uoni hafifu pamoja na kukosa mafuta maalumu ya kulinda ngozi pamoja na elimu ndogo kwa jamii kuhusu ualbino." Amesisitiza Enos.
Mdahalo huo wa kupinga mauaji ya watu wenye Ualbino Mwanza umefanyika kwa ushirikiano baina ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mwanza (MPC) na Chama cha Jamii ya watu wenye Ualbino (TAS) Mdahalo uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.