Chama cha wasioona Tanzania (TLB) kimesema kuwa hakina tatizo na uongozi wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kutokana na changamoto zilizokuwa zinazokikabili chama hicho kupungua siku hadi siku.
Kauli hiyo imetolewa jijini hapa na Mwenyekiti wa Chama cha Wasiona Tanzania Mkoa wa Mwanza Musa Mashauri juu ya maandalizi ya maadhimisho ya fimbo nyeupe ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Mwanza.
Mashauri amesema TLB inamshukuru Rais John Magufuli kwa upendo wa dhati kwa watu wenye ulemavu wa kutoona na walemavu wengine nchini kwa kuwathamini na kufanya maamuzi stahiki ya kumteua mmoja wa walemavu Amon Mpanju kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
“Niseme tu sisi tunamshukuru sana Rais wetu mpendwa, anatujali na anatuthamini, nasema na mwandishi kaandike hivyo kwamba sisi hatuna shida na rais wetu kwa sasa tunampenda kwa jinsi anavyotujali,”alisema.
Akizungumzia maandalizi ya maadhimisho hayo yatakayoadhimishwa kwa kauli mbiu, “ Mafunzo ya Tehama kwa wasioona ni nyenzo jumuishi katika uchumi wa viwanda,” alisema maandalizi muhimu yamekamilika.
Alisema uamuzi wa maadhimisho hayo kitaifa kufanyika mkoani Mwanza ulifikiwa baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya TLB kwenye kikao chake kilichofanyika mjini Morogoro kuja na uamuzi huo.
Alisema tangu wakati huo shughuli mbalimbali za maandalizi zimekuwa zikifanyika kwa ajili ya kufanyika maadhimisho hayo, ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Furahisha ambayo kilele chake ni Oktoba 25 mwaka huu.
“ Mfano tuliwasilisha barua kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella kuomba mkoa wake kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya kitaifa na alilikubali ombi letu,” alisema.
Alisema kwa msaada wa Mongella, imeundwa kamati maalum ya mkoa ya watu 20 ambayo imepewa jukumu la kuratibu maadhimisho hayo ambayo inaongozwa na Katibu Tawala Msaidizi (Miundombinu) Seif Hussein.
“ Kamati hiyo imetengeneza mpango kazi wa bajeti kwa ajili ya maadhimisho hayo, ambapo jumla ya Sh. milioni 74 zinahitajika, lakini kutokana na michango ya vifaa kwa ajili ya watu wasioona, naweza kusema tumepata karibu asilimia 80 ya lengo ”, alisema.
Aliwashukuru watu waliosaidia kufanikisha michango hiyo ikiwemo serikali ya mkoa wa Mwanza, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mkurugenzi wa the Desk and Chair Foundation Sibtain Meghjee na wadau wengine wanaoshirikiana nao Mobiles Eyes Foundation Tanzania, Beta Charitable Trust, Flora na Bilal Muslim Tanzania ambao kwa pamoja wamechangia vifaa mbalimbali vya tiba, zikiwemo fimbo nyeupe, miwani na vifaa vya upasuaji vyenye thamani ya Sh milioni 20.
“ Lakini pia kupitia maadhimisho haya, tumefanikiwa kuandaa siku ya macho, ambapo wananchi wenye matatizo ya macho watapata huduma bure ya upimaji wa macho na tumeandaa maonesho ya wajasiriamali kwa wasioona lengo likiwa ni kuionyesha jamii kuwa wasioona sio ombaomba na wao wanaweza kufanya kazi na kujipatia kipato,” alifafanua.
Alisema kutokana na ufinyu huo wa bajeti, baadhi ya shughuli ambazo zilipangwa kufanyika kwenye maadhimisho hayo zimeondolewa. Alizitaja shughuli hizo zilizoondolewa kuwa ni upandaji wa miti 400 kwa ofisi za wakuu wa wilaya za Nyamagana na Ilemela, Shule Maalum ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ya Mtindo iliyoko wilayani Misungwi.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Philis Nyimbi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkurugenzi wa the Desk and Chair Foundation Sibtain Meghjee alisema wametoa vifaa hivyo kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt.Philis Nyimbi aliishukuru taasisi ya the Desk and Chair Foundation kwa moyo wako wa upendo wa kuwajali watu wenye ulemavu na mahitaji yao na kuyaomba mashirika na wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano wao.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) Dkt.Silas Wambura akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, alithibitisha kuwa vifaa hivyo vinafaa kwa huduma za utoaji wa tiba na kinga kwa jamii ya watu wasiiona nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi hayo Seif Hussein alisema maandalizi kwa ajili ya maadhimisho hayo yamekamilika na kwamba Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia ulemavu Mhe.Stela Ikupa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.