Serikali imetenga kiasi cha Sh milioni 960 kwa ajili ya uboreshaji wa mradi wa utambuzi wa mahali, hatua itakayoiwezesha kutoa huduma muhimu kwa wananchi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa maisha yao.
Hayo yamesemwa jijini hapa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi Dkt. Jim Yonas ambaye yuko katika ziara ya kukagua na kuona jinsi mradi maalum wa utambuzi wa maeneo unavyotekelezwa katika jiji la Mwanza.
Alisema fedha hizo ambazo zinatokana na mapato ya ndani zimetolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi muhimu wa utambuzi wa maeneo ambao sasa kila mtaa utatambuliwa kwa jina lake na hivyo kuiwezesha serikali kufahamu mahitaji muhimu ya maeneo yanayotokana na huduma muhimu za kijamii kama vile afya, elimu na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi na ukuaji wa uchumi.
“ Nia ya serikali katika mradi huu ni kuhakikisha kuwa kila sehemu inatambuliwa kwa kupewa alama yake ya utambulisho “ Post code” ili pamoja na mambo mengine kuiwezesha serikali kujua ikama kamili ya watu, ikiwemo wafanyabiashara ili iweze kukusanya kodi,” alisema na kuongeza kuwa mradi huo wa utambuzi wa maeneo utaboreshwa zaidi ikiwa ni pamoja na taarifa za mradi huo zitapatikana pia kwenye vitambulisho vya taifa na hauna tofauti na mradi wa utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama “ Wamachinga."
Alisema tayari utekelezaji wa mradi huo umeanza kutekelezwa vyema katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na lengo ni kutekelezwa kwa mikoa yote nchini kwa kushirikiana na halmashauri za miji,majiji na wilaya ambazo zitatengeneza sheria ndogo kwenye maeneo yao lengo likiwa ni kuhakikisha mradi huo unatekelezwa vyema kwa mikoa na halmashauri, manispaa na majiji yote nchini.
“Tanzania imeamua kupitia mradi huu muhimu kuhakikisha kuwa mradi huu wa utambuzi wa maeneo unachochea ukuaji wa uchumi, lengo tutahakikisha kuwa kila kata inakuwa na post code na kwa mradi huu maana yake tunaifungua Tanzania ili ishiriki kwenye shughuli za kiuchumi ,” alisema na kuongeza kuwa serikali itaendelea kutoa fedha kwa awamu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na halmashauri kwa upande wao nazo zitajenga bajeti kwenye maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji na uendelevu wa mradi.
Alisema kukamilika kwa mradi huo utasaidia pia katika shughuli za uokoaji wa majanga ya moto ambapo kwa sasa itakuwa ni rahisi kwa mamlaka zinazodhibiti moto kupewa taarifa ya eneo na mtaa ambao kuna janga la moto.
“ Kabla ya hapo, haikuwa ilikuwa mtu anayeenda kudhibiti moto anaambiwa kata kona mara kushoto bila ya kujua moto uko eneo gani, kumbe uko mtaa wa saba, haya ndiyo maendeleo tunayotaka,’’ alisisitiza.
Ameipongeza kamati maalum ya utekelezaji wa mradi huo kwa halmashauri ya jiji la Mwanza kwa kuanza vizuri zoezi la utekelezaji wa mradi huo, ambapo jumla ya vifaa ambazo ni nguzo 423 na mbawa 747 zimeanza kuwekwa kwenye maeneo kwa ajili ya utambuzi rasmi wa maeneo na mitaa ambayo yatapewa majina rasmi.
“Niipongeze sana timu ya Mwanza kwa kazi kubwa iliyofanya, nadhani nitarudi tena huku ili kuona utekelezaji wa mradi huu,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba aliishukuru serikali kwa ajili ya kutoa fedha kiasi cha Sh milioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambapo alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa mradi huo utatekelezwa kwa muda uliopangwa.
“Suala la Post code sio tu linataka kurahisisha mawasiliano na kupendezesha jiji letu, lakini tunakwenda kuboresha uchumi wetu,” alisema na kuongeza kuwa mradi huo utaiwezesha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kukusanya mapato yake kutokana na kuwa na utambuzi rasmi wa maeneo na ikama ya makundi maalum ya watu, yakiwemo ya wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo na ujumbe wake waliitembelea pia manispaa ya Ilemela ambapo nako ameupongeza uongozi wa manispaa ya Ilemela kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa ajili ya ustawi wa wananchi na ukuaji uchumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.