Mkoa wa Mwanza umetangaza rasmi mkakati madhubuti maeneo yote ya vivuko,bandari pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa wa jijini Mwanza,kwa wageni wote wanaoingia mkoani humo kutoka nje ya nchi kufanyiwa vipimo ili kubaini kama wameathirika na homa ya mafua makali yanayosababishwa na kirusi aina ya corona.
Afisa Afya Mkoa wa Mwanza Fungo Masalu akizungumza wakati wa kujadili masuala ya lishe,afya ya uzazi hususani kwa mama mjamzito,mtoto pamoja na tahadhari ya magonjwa ya homa ya manjano na homa ya mafua makali yanayosababishwa na kirusi kipya aina ya corona yanayoendelea katika nchi mbalimbali alisema, mkakati uliopo ni kuimarisha mipaka ambayo inaingiza wageni.
“Tumeweka utaratibu wa kupima joto la mwili endapo mtu akiwa na joto homa kali atafanyiwa uchunguzi kubaini alipotokea yawezakuwa ametokea nchi iliyoathirika kwa sababu hali yake imeashiria kuwa na ugonjwa”alisema Masalu.
Aliongeza kuwa elimu ya afya itatolewa kwa umma hususani kipindi hiki kabla ya ugonjwa kufika nchini ili waweze kuzingatia kanuni za afya katika kujikinga na ugonjwa huo.
Awali ya yote Mratibu wa huduma ya mama na mtoto Mkoa wa Mwanza Cecilia Mrema,akitoa taarifa ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto na hali ya vifo vya wazazi alisema, kwa mwaka jana mama wajawazito waliopoteza maisha kwa kutokwa na damu nyingi pamoja na kifafa cha mimba wakati wa kujifungua walifikia asilimia 40, hivyo wameweka mkakati ili kumaliza tatizo hilo ambapo hatua ya kwanza ni kuhakikisha upatikanaji wa damu unakuwa wa uhakika wakati wote.
Pia aliwataka wajawazito wote kupima wingi wa damu mapema ili ikibainika anakiwango kidogo cha damu waweze kumsaidia mapema akiwa kwenye huduma za wajawazito kabla ya wakati wake wa kujifungua endapo akichelewa hatutaweza kumsaidia katika hatua ya mwisho.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Dkt.Emmanuel Kipole kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella,alisema umasikini wa kipato,machafuko ya kisiasa na sera zisizo tambua umuhimu wa lishe ndio chanzo kikubwa cha jamii kuwa na lishe duni.
Pia uelewa huo mdogo wa masuala ya lishe umechangia suala hilo kutokupewa kipaumbele katika mipango na bajeti hususani katika ngazi za halmashauri ambapo ndipo walipo watoto, vijana na wanawake wanaohitaji huduma bora za lishe .
“Serikali kwa kutambua lishe ni suala la kimaendeleo hapa Tanzania mapambano dhidi ya lishe duni yamekuwa ni moja wapo ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ulianza mwaka 2016-2017 na 2020-2021,”alisema Kipole.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.