Kuna msemo usemao “Maji ni uhai” , Katika hali ua kawaida msemo huu hutumiwa na watu mbalimbali wakiashiria umuhimu wa raslima hiyo muhimu kwa ustawi wa maisha yao.
Hubainika kuwa ni msemo ambao hauna tija, hasa pale kunapotokea tatizo la uhaba wa maji visimani na kwenye mabomba ya maji, hali inayoifanya jamii, wakiwemo wanawake kuhangaika kutafuta maji.
Hali hiyo ya kukatika kwa maji mabombani katika maeneo ya mijini ama kukauka visimani kwenye maeneo ya vijijini ndiyo hudhihirisha umuhimu wa maji katika jamii.
Maji pia ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii duniani. Maji pia hutumiwa kwenye shughuli za viwandani, hosipitalini, taasisi /shule, wananchi wenyewe na katika baadhi ya mitambo iliyopo sehemu mbalimbali duniani.
Pamoja na umuhimu huo wa maji,bado hakuna uwiano sawia wa mgawanyo wa maji kati ya sehemu moja na nyingine, kutokana na mabadiliko ya majira mbalimbali ya mwaka kutegemeana na eneo husika na hali ya upatikanaji wa maji.
Maji haya pia yamekuwa yakipungua siku hadi siku kutokana na kuongezeka kwa mahitaji. Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita mahitaji ya maji yameendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa.
Hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya ongezeko ya idadi ya watu, uzalishaji mali kwenye sekta za umwagiliaji, uzalishaji viwandani,uchimbaji wa madini, ufugaji na matumizi mengine muhimu yanayohitaji maji.
Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inaeleza bayana kuwa mfumo wa sasa wa usimamizi na matumizi ya raslimali za maji ,bado haukidhi mazingira ya mahitaji ya upatikanaji wa maji.
Kwa mujibu wa sera hiyo asilimia 90 ya Wakazi wa mijini ndio hupata huduma ya maji na maeneo ya vijijini ni asilimia 60-75 tu,hali hii inadhihirisha kuwa huduma ya maji bado inahitaji zaidi hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Ni kwa mantiki hiyo basi, Mkoa wa Mwanza umeamua kuja na mikakati kabambe ya kisayansi ya kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa.
Katika kufanikisha azma na lengo hilo, mkoa wa Mwanza umeendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wa uboreshaji wa huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 53.4 mwaka 2015 hadi asilimia 70 kwa mwaka 2020 ili kuendelea kutekeleza lengo la kuwapatia maji wananchi wa vijijini, Meneja wa wakala wa maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza Mhandisi Waryoba Sanya anasema katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, jumla ya miradi 72 ya maji katika mkoa imeendelea kutekelezwa.
Anaitaja baadhi ya miradi hiyo ya usambazaji maji ya bomba (piped water projects) ni Igombe –Kabusungu Ilemela); Bitoto –Buyagu (Sengerema); Matela –Nyanguge (Magu) ; Kalebezo (Buchosa) na Misasi –Ngaya (Misungwi) na Shilima - (Kwimba).
“Miradi hii ina lengo la kuendelea kuboresha upatikanaji maji safi na salama vijijini ambapo sasa upatikanaji maji ni asilimia 59. Juhudi zinafanywa kuhakikisha miradi inayoendelea kujengwa inapata fedha na kusimamiwa na hivyo kukamilika kabla ya Juni 2020,”anaeleza.
Katika lengo mkoa la ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 93,051 vitakavyohudumia watu 23,262,876 ambavyo vitaongeza idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama kutoka 20,022,283 mwaka 2015 hadi kufikia 43,285,159 mwaka 2020 sawa na asilimia 53.7, anasema jumla ya vituo vya kuchotea maji (water points) 2,319 (Sengerema -352, Buchosa -159; Kwimba - 1,294 na Misungwi - 524), Ilemela -25, Magu- vituo 17 vimejengwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni 2019 kwa lengo la kusogeza huduma ya maji kwa wananchi.
Kwa upande wa upatikanaji wa huduma za maji katika miji mikuu ya mikoa kutoka asilimia 86 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 95 ifikapo 2020, anasema Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Taka (Mwauwasa) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ili kuongeza upatikanaji wa maji mijini.
“Kwa sasa huduma ya maji jijini Mwanza imefikia asilimia 90 ya wakazi wanaoishi mjini kati wanapata huduma ya maji safi,” anasema na kuongeza kuwa watu wanaoishi maeneo ya pembezoni ya Jiji wameandaliwa miradi mipya inayojengwa sasa ikiwemo ya Mradi wa maji miji ya wilaya ya Misungwi na Magu ambayo ipo mbioni kukamilika na vilevile miradi ya mitaa ya Kabusungu, Igombe, Nyafula, Nyamwilolelwa, Kayenze, Ibanda, Lwanhnima.
Anasema ujenzi wa mradi mkubwa wa chanzo kipya kipya cha maji cha Butimba utakaojenga matenki mapya ya kuhifadhi maji mengi maeneo ya Buswelu na Mkolani na hivyo kuwezesha maji kufika maeneo ya pembezoni ya Jiji la Mwanza na Usagara wilayani Misungwi.
“Pia mradi wa kujenga matenki makubwa mapya maeneo ya milimani ikiwemo Nyasaka-Jeshini, Bugarika, Kirumba na upanuzi wa njia za maji unafanyika sasa na unatarajiwa kukamilika Mwezi Juni 2019,” anasema na kuongeza kuwa miradi hiyo itaongeza upatikanaji wa maji kufikia asilimia 97 mwaka 2020.
Katika lengo la mkoa la kuongeza upatikanaji wa huduma za maji katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na maeneo ya miradi ya Kitaifa kutoka asilimia 57 mwaka 2015 hadi kufikia asilimi 90 mwaka 2020, anasema hali hiyo imeendelea kuimarishwa ambapo upatikanaji wa maji katika miji mikuu ya wilaya iko katika hatua ya kuridhisha. Upatikanaji huo ni kama ifuatavyo kwa asilimia Ukerewe - Nansio (85), Sengerema (82), Kwimba- Ngudu (63), Misungwi (49) na Magu (44).
Anasema utekelezaji wa miradi ya maji unaoendelea kwenye miji mikuu ya Magu na Misungwi upo katika hatua za ukamilishaji ifikapo Agosti 2019 na utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji hadi wastani wa asilimia 90 kwenye miji hiyo kufikia mwaka 2020.
Kwa upande wa ukamilishaji wa miradi mikubwa ya maji na kuhakikisha vijiji vyote vilivyopo kandokando ya miradi hiyo mikubwa vinanufaika, anasema kupitia mradi wa Maji kutoka ziwa Victoria kwenda Kahama - Shinyanga (KASHUWASA), miradi minne inaendelea kujengwa katika Wilaya za Kwimba 2 (Igungunya –Nyahiga na Shilima –Mahande -Izizimba) na Misungwi miradi miwili ( Mbarika –Ngaya na Matale – Manawa- Misasi ) imejngwa ili kuongeza upatikanaji wa maji ambapo miradi hiyo imekamilika na itazinduliwa muda wowote kuanzia sasa.
Anaongeza kuwa kwa sasa MWAUWASA wamekabidhiwa na Waziri wa Maji Mhandisi Isaac Kamwele kukamilisha miradi ya maji ya Shilima –Izizimba baaada ya mkandarasi wa awali kushindwa.
“Hata hivyo, Vijiji 11 vilivyopo wilayani Kwimba na Misungwi vimenufaika na mradi huu baada ya kukamilika,” anasema.
Katika kukamilisha ukarabati wa mabwawa ambayo tayari yamekwishajengwa, anasema bwawa la Malya lililoko wilayani Kwimba limeendelea kufanyiwa ukarabati ili kutoa huduma ya maji safi kwa mji wa huo na pia Serikali tayari imejenga bwawa la maji katika kijiji cha Mahiga.
Katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana Kwenye vijiji vinavyozunguka ziwa Victoria, Sanya anasema jumla ya miradi 69 inaendelea kujengwa mkoani Mwanza na kazi ya usanifu wa miradi mipya ya maji katika vijiji vinavyozunguka ziwa katika wilaya za Ilemela, Buchosa, Sengerema na Misungwi unaendelea.
“Mkoa umetekeleza miradi ya visima virefu vinavyotumia nishati ya jua 564 katika wilaya za Buchosa-34, Sengerema-82, Kwimba-199, Misungwi-35,Magu-176, Ilemela-38, visima vitano Sengerema tayari vimefungiwa pampu za mkono,” anasema.
Anasema unaendelea kuhamasisha wananchi kuunda Jumuiya za Watumia Maji Vijijini katika Mabonde yote ya maji nchini ifikapo mwaka 2020 ili kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika kupanga, kujenga ,kuendesha na kumiliki miradi ya maji, ambapo jumuiya za watumiaji maji 385 zimeundwa kwa wilaya zote za mkoa wa Mwanza-(Sengerema 68; Kwimba 37; Misungwi 15; Magu 265 ).
“Na kwa utaratibu mpya wa kuundwa wakala wa maji Vijijini (RUWASA) wataendela kuimarisha utoaji wa huduma hii, faida ya jumuiya hizi zimewezesha kusimamia utoaji wa huduma ya maji vijijini kuwa endelevu na kuondoa migogoro katika vyanzo vya maji na utumiaji raslimaji,” anaeleza
Kuhusu miundombinu ya majitaka, anasema Serikali imeendelea kujenga miundombinu ya maji taka na kuimarisha utoaji wa maji taka Jijini Mwanza na miji ya makao makuu ya Wilaya.
Aidha, anaongeza kuwa huduma ya uondoshaji wa maji taka katika Jiji la Mwanza inaendelea kwa kutumia mfumo wa bomba la maji taka (Sewarage System network) wenye urefu wa Km. 87.7 kupitia MWAUWASA, ambapo huduma hii inahudumia asilimia 30 ya mji .
Anasema maeneo yaliyobaki hasa nje ya Jiji na Wilaya uondoshaji majitaka unafanywa kwa kutumia magari ya majitaka, ambapo miradi mipya miwili ya kuondoa maji taka imejengwa katika maeneo ya makazi horera/yasiyopangwa milimani ya Kiloleli na Mabatini na kuwa bora na ya mfano kwa nchi nzima.
“Uandaaji wa mipango na usanifu wa kupanua mradi huu umeendelea kufanyika kwa ajili ya miundombinu ya majitaka mipya katika maeneo yenye changamoto za makazi horera/yasiyopangwa,” anasema.
Aidha, anasema magari ya kunyonya maji taka yamenunuliwa na ujenzi wa mabwawa ya kuhifadhi maji taka yamejengwa katika miji ya makao makuu ya Wilaya za Nansio-Ukerewe na Sengerema.
Kwa upande wa miradi inayotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) jijini Mwanza, infanyika kwa kasi kupitia Programu ya uboreshaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza, Miji ya Bukoba na Musoma, Miji Midogo ya Misungwi, Magu na Lamadi.
Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele anasema mamlaka yake imepata mafanikio makubwa kutokana na miradi ya uboreshaji huduma za maji katika miji ambayo imelengwa katika program hiyo chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Washirika wa Mashirika wa Maendeleo ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank)
Anasema miradi inayotekelezwa kupitia programu hiyo ya uboreshaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza na miji mingine ni mji mdogo wa Misungwi, Magu na Lamadi na inatekelezwa chini ya Ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Washirika wa Maendeleo ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank, EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (Agence Francaise de Development, AFD) kwa gharama ya shilingi bilioni 276.925 sawa na euro milioni 104.5.
Anabainisha kuwa ni kutokana na ufadhili wa EIB na AFD kupitia mkopo wenye masharti nafuu ambapo EIB inachangia shilingi bilioni 119.25 sawa na euro milioni 45 wakati Serikali ya Tanzania inachangia shilingi bilioni 38.425 sawa na euro milioni 14.5.
Anabainisha kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya Jiji la Mwanza ni k shilingi bilioni 140.37 sawa na euro milioni 52.97, miji ya Bukoba na Musoma imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 77.645 sawa na euro milioni 29.30 na miji midogo ya Misungwi, Magu na Lamadi kwa pamoja imetengewa shilingi bilioni 42.64 sawa na euro milioni 16.09.
“Kiasi cha shilingi bilioni 16.27 (euro milioni 6.14) sawa na asilimia 5.88 ya gharama zote za miradi zinatumika katika usimamizi wa mradi,” anasema.
MRADI WA KUBORESHA HUDUMA YA MAJI SAFI NA MAJITAKA
Anasema kuwa gharama za mradi huu ni euro14,689,448.35 sawa na shilingi bilioni 38.927, ambapo shughuli za ujenzi wa mradi huo zinatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya M/s. JOS. HANSEN & SOEHNE GmbH in JV with M/s. JR INTERNATIONAL BAU GmbH kutoka Ujerumani.
Anasema mkataba wa utekelezaji wa shughuli za mradi huo ulisainiwa Februari 16 mwaka juzi kati ya MWAUWASA na Mkandarasi na utekelezaji wa kazi za ujenzi wa mradi zilianza rasmi Mei 26, mwaka juzi.
KAZI ZINAZOTEKELEZWA NA MWAUWASA
Mhandisi Msenyele anafafanua kuwa kazi zinazotekelezwa na MWAUWASA ni uboreshaji na kupanua huduma ya majisafi katika maeneo ya milimani hususani maeneo yaliyo juu ya matenki ya maji ambayo hayapati huduma kwa sasa ambayo ni Nyasaka, Bugarika, Nyegezi, Capripoint, Mjimwema, Nyakabungo na Kitangiri.
Anasema shughuli za mradi ambazo kwa sasa zinaendelea ni pamoja na ujenzi wa matenki ya maji katika maeneo ya Kitangiri (tenki moja la lita 500,000), Nyasaka (tenki moja la lita 1,000,000), Mjimwema (tenki moja la lita 1,200,000), Nyegezi (tenki moja la lita 1,200,000) na Bugarika (matenki mawili ya lita 700,000 na 250,000).
“ Pia tunaendelea na kazi za utandazaji wa bomba za kusafirisha na kusambaza maji zenye vipenyo kati ya milimita 315 na milimita 50 jumla ya urefu bomba hizo ni mita 64,820,” anasema na kuyataja maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni Kitangiri, Kiseke, Nyasaka, Nyegezi, Bugarika, Mahina, Isamilo, Mjimwema/Nyakabungo na Nyankurunduma.
Kuhusu uboreshaji wa huduma ya majisafi kupitia ubadilisha wa mabomba ya zamani yaliyochakaa na kuongeza mtandao wa mabomba, anasema kazi hiyo inafanyika katika maeneo ya Makongoro, Nyakato na Barabara ya Kenyata (Jumla ya urefu wa mabomba ni mita 15,770) na jumla ya mita 2,000 za mtandao wa mabomba zitaongezwa katika eneo la Makongoro.
Kazi nyingine kwa mujibu wake ni kubadilisha viungio katika mtandao wa majisafi - "Valves and Fire hydrants" kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kusambaza maji na kuongeza wigo wa kitengo cha Zimamoto kukabiliana na majanga ya moto na jumla ya vifaa hivyo ni 22.
Anasema shughuli zingine zinazoendelea ni pamoja na kuboresha na kupanua mfumo wa majitaka kupitia utandazaji wa mabomba mapya na ubadilisha wa mabomba ya zamani yaliyochakaa ambapo mabomba yenye jumla ya urefu wa mita 4,775 na vipenyo kati ya 600mm na 225mm yatatandazwa.
“Kazi hiyo inafanyika katika maeneo ya Mabatini “A” & “B”, Kilimahewa, Isamilo, Igogo, barabara ya Kenyatta na Makongoro. Pia kuongeza ufanisi wa mitambo ya kusukuma majitaka katika kituo cha Makongoro, Kirumba na Mwanza South,” anasema.
Anasema mradi huo ambao tekelezaji wake umefikia asilimia 90 ambapo hadi kufikia Machi 31 2019, utekelezaji wa Shughuli za Mradi ulikuwa umekamilika kwa asilimia 75 na pindi utakapokamilika, mradi huo utanufaisha wakazi wapatao 105,649 waishio katika maeneo ya Jiji la Mwanza yaliyotajwa hapo juu na hiyo ni kwa tathimini ya mpaka kufikia mwaka 2028.
MRADI WA KUBORESHA HUDUMA YA MAJISAFI
Anasema utekelezaji wa mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Midogo ya Misungwi, Magu na Lamadi unatekelezwa kama sehemu ya Programu ya Kuboresha Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji hii Midogo (Misungwi, Magu na Lamadi).
Anasema shughuli za ujenzi wa mradi huo katika miji yote mitatu zinatekelezwa na Kampuni ya M/s. CHINA CIVIL ENGINEERING CONSTRUCTION CORPORATION (CCECC) kutoka China kwa Mkataba mmoja wenye thamani ya euro 16,096,951.21 sawa na shilingi bilioni 42.657 ambazo ni gharama za jumla za mradi kwa Miji yote mitatu (3).
Anasema gharama za mradi huo kwa mji mdogo wa Misungwi ni euro. 4,850,914.54 sawa na shilingi bilioni 12.855, Magu ni euro. 6,404,169.56 sawa na shilingi bilioni 16.971 na Lamadi euro. 4,841,867.11 sawa na shilingi bilioni 12.831.
Anasema mkataba wa utekelezaji wa shughuli za mradi ulisainiwa Februari 16, 2017 kati ya MWAUWASA na Mkandarasi, ambapo utekelezaji wa kazi za ujenzi wa mradi zilianza rasmi Mei 22 2017 kwa miji yote Mitatu na umekamilika kwa asilimia 85 na hadi kufikia Machi 31 2019, utekelezaji wa shughuli za mradi huo katika miji yote mitatu ulikuwa umekamilika kwa wastani wa asilimia 83.
WANANCHI WAFURAHIA UJENZI WA MIRADI YA MAJI
Mosi Richard mkazi wa Mabatini jijini Mwanza anaishukuru serikali kwa kuwezesha ujenzi wa miundombinu maji ya kisasa katika eneo la Mabatini iliyowezeshwa kupatikana sasa huduma ya maji ya bomba kwa wananchi.
“ Serikali imefanya kazi kubwa, sasa tumeyaona maji ingawa iboreshe maana kuna wakati yanakatika,” anasema
Kwa upande wake Godfrey Maiko mkazi wa Nyakato anasema serikali ya awamu ya tano imejipambua kwa wananchi wanyonge, ambao kwa sasa karibu maeneo mengi ya jiji la Mwanza wananchi wanapata huduma za maji.
Kwa upande wake Godfreu Kiswene mkazi wa jijini Mwanza anasema maji katika jiji la Mwanza sasa ni raha tupu na kwamba ile kero ambayo wananchi waliyokuwa nayo imetoweka ingawa kwa baadhi ya maeneo machache huduma huwa maji yanakatika.
“ Niiombe Serikali yangu iendelee kuboresha huduma za maji ili maji yamiminike kwa wingi kwa wananchi,” anasema Kiswene.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.