Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa wazee kula vyakula vyenye lishe bora kwa kufuata mlo kamili na kuzingatia makundi yote muhimu ili kujihakikishia afya imara na kuepuka maradhi hususani yasiyoambukiza.
“Wazee tuache tabia ya kula vyakula bila kufuata mlo kamili kwa mfano mtu asubuhi anakula wali, mchana anakula wali na usiku pia anakula wali wakati huo ni wanga ambao kazi yake ni kuleta nguvu na kubadilika kuwa sukari na mafuta hivyo ni vyakula ambavyo havitusaidii kwa afya yetu.” Mhe. Mtanda.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo leo tarehe 29 Septemba, 2025 wakati akihutubia katika kongamano la Siku ya Wazee duniani lililoadhimishwa kimkoa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwakutanisha wazee zaidi ya 200 waliojadili kuhusu mustakabali wa maisha yao.
Aidha, amewahakikishia wazee hao kuwa serikali itaendelea kuboresha maisha yao katika nyanja mbalimbali kama kuwapatia huduma bora za afya bila malipo ambapo akabainisha jumla ya wazee Elfu 97 wametambuliwa na kupewa vitambulisho mkoani humo.
Kadhalika, amewasihi kundi linaloelekea kwenye uzee kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali kama kilimo, uvuvi na ufugaji ili kujiwekea akiba ya uchumi imara wakati wa uzee jambo litakalowasaidia kuondokana na msongo wa mawazo.
Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Jesca Lebba amesema Mwanza yenye vituo 569 vya kutolea huduma unatoa kipaumbele kwa kundi hilo na kwamba jumla ya wazee elfu 78 wamehudumiwa 2024/25 na kupitia mabaraza ya wazee halmashauri zinawawezeshwa kwa kuwahusisha na shughuli mbalimbali za uchumi.
Akiongea kwa niaba ya mwenyekiti, Mzee Juma Ngeleja ametumia wasaa huo kuishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za kijamii kama kujengwa kwa zahamati vijijini na uwepo wa madawati maalumu ya kuwahudumia kwa kipaumbele kwani ni ishara kuwa serikali inajali afya ya wazee.
Oktoba Mosi ya kila mwaka ni siku ya wazee duniani ambapo kitaifa hapa nchini siku hiyo itaadhimishwa kesho kutwa mkoani Ruvuma chini ya Kaulimbiu isemayo ‘Wazee tushiriki uchaguzi Mkuu 2025 kwa ustawi wa jamii yetu’.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.