Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amewataka wajumbe wa Kamati za Utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa Kuzuia na kupambana na Rushwa kutumia mfumo wa E-Maboresho kwa ufanisi ili kusaidia kumaliza tatizo la Rushwa nchini.
Ametoa rai hiyo leo tarehe 09 Oktoba, 2025 wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa utekelezaji wa mkakati wa IV wa kitaifa wa kuzuia na kupambana na Rushwa yaani E-Maboresho katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Amesema, serikali inatamani kuona rushwa imetokomezwa kabisa nchini ili kuhakikisha taifa linasonga mbele kwa mujibu wa katiba ya nchi, hivyo matumizi ya mfumo huo yatawaimarisha wajumbe wa kamati kuweza kuchakata taarifa na kuwasilisha kwa wakati kwa ajili ya hatua zinazofuata.
Aidha, Bw. Balandya amemithilisha uboreshwaji mkubwa wa miradi ya maendeleo katika sekta za miundombinu, Elimu, Maji, Afya, Kilimo, Uchukuzi na Miundombinu na mafanikio ya mikakati ya kupambana na rushwa kwani imeleta matumizi mazuri ya fedha kwenye miradi.
Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka OR Ikulu Bi. Christina Maganga amebainisha kuwa mafunzo hayo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuzuia Rushwa E-Maboresho yamelenga kuwajengea uwezo Wenyeviti na Makatibu wa Kamati hizo pamoja na Maafisa TEHAMA.
Aidha, amefafanua kuwa mafunzo hayo yalikwishafanyika katika mikoa 17 ukiwemo Mkoa wa Mwanza na kwamba kwa siku mbili hizo yamewakutanisha wajumbe kutoka mikoa ya Mara, Simiyu na Kagera ambao watajengewa uwezo juu ya utumaji wa taarifa za utekelezaji wa kila robo kuhusu masuala ya mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa ili maamuzi yatolewe kwa wakati.
Wakati akijinasibu na uwepo wa vivutio lukuki vya utalii mkoani humo na kuwahamasisha kuvitembelea wawapo kwenye mafunzo hayo, Katibu Tawala amewasihi wajumbe wa mafunzo hayo kuhakikisha wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.