Mkoa wa Mwanza wametumia siku ya tarehe 27 Januari, 2026 ambayo ni Siku ya Kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupanda miti 16,000 katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo chini ya ushirikiano na Wakala wa Misitu nchini (TFS).

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Said Mtanda baada ya kushiriki zoezi la upandaji Miti zaidi ya 1200 katika Shule mpya ya Sekondari Kakebe- Igoma wilayani Nyamagana akiwa anahitimisha zoezi hilo aliloanza kwa kupanda Miti katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela.

Mhe. Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza umeungana na Mhe. Rais kufanya kazi za kijamii kwa kupanda miti ya matunda ili kwenda sambamba na afua ya lishe bora wa watoto kwa siku za baadaye pamoja na kusaidia katika uhifadhi wa mazingira.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kupanda miti kwenye mashamba na hata katika mazingira ya makaazi ili si tu kupanda miti bali kufanya sadaka kwa Mwenyezi Mungu kwa kujenga taifa la kijani kwa siku za usoni.

“Suala la kuhifadhi mazingira ni la kizalendo, mazingira bora yatajenga maisha bora na jamii ikihifadhi vizuri tutapata mvua za kutosha hivyo niwatake wananchi wote kupanda miti kwenye kaya zenu,” amesema Mkuu wa Mkoa.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema pamoja kupanda miti katika Shule hiyo Wilaya imehamasisha upandaji miti katika maeneo yote hadi kwenye kaya na kwamba wanapanda miti ya matunda ili isiwe tu kwa ajili ya kivuli bali kuhamasisha lishe bora.

Aidha, ametumia wasaa huo kuishukuru Serikali kwa kuleta fedha nyingi za miradi huku akijinasibu kuwa upandaji miti kwenye shule hiyo mpya ya Kakebe utasaidia kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea zaidi ya Kilomita 5 kutoka Shamaliwa kwenda Igoma.

Mhe. Mkuu wa Mkoa amechagiza hafla ya upandaji miti kwa kuendesha harambee kwa ajili ya kupata fedha Tshs. 1,800,000 za kuunganisha umeme na Maji kwenye shule hiyo ambapo zimepatikana Tshs. 1,350,800 papo hapo na amemuagiza Meneja wa TANESCO kupeleka umeme mara moja huku Maji yakifuata kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji hilo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.