Jumla ya wasichana 31291 Mkoani hapa wenye umri wa miaka 14, wanatarajia kupatiwa chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi.Chanjo hiyo itahusisha mabinti kutoka katika wilaya zote za Mkoa wa Mwanza walioko shuleni 26,641 na walio nje ya shule 4,650.
Akizungumza na wananchi pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mkuyuni C waliofika hospitali ya Nyamagana kwa ajili ya kupata Chanjo hiyo, Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Silas Wambura alisema uzinduzi wa chanjo hii umefanyika leo april 23 katika hospitali ya wilaya ya Nyamagana Butimba ila chanjo itaendelea kwa vituo vyote na itakuwa ni bure.
“Chanjo hii itaenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya chanjo kitaifa ambayo yameanza leo April 23 hadi 30, pia chanjo hii imelenga mabinti kuanzia umri wa miaka 9 hadi 14 kwa ajili ya kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi ambayo imekuwa ni tatizo kwa wanawake nchini na duniani kote,” alisema Dkt.Wambura.
Pia aliongeza kuwa, kutokana na serikali kutokuwa na uwezo wa kugharamia chanjo hizo kwa sasa imeamua kuanza na mabinti wenye umri wa miaka 14 ila kadri wanavyo endelea wataanza kutoa kwa mabinti wenye miaka 9 hadi 13, na ndoto yao hapo baadae Nchi iweze kutengeneza chanjo hizo na dawa kama ilivyo dhamira ya Rais wa Jamuhuri ya Muungangano wa Tanzania ya kuifanya kuwa ni nchi ya viwanda.
Aidha,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. alisema, mbali na chanjo hiyo pia kutakuwa na chanjo ya polio kwa njia ya sindano kwani mwanzo ilikuwa ya matone hivyo aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwani chanjo hiyo ni salama na haina madhara kwa binadamu na imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani(WHO) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mwanza Amos Kiteleja alisema, saratani ya shingo ya kizazi ina athari kubwa kwa afya ya wanawake ulimwenguni kote na inakadiriwa kila mwaka wanawake 466,000 wanathibitika kuwa na ugonjwa huo na wengi wao wako katika nchi zinazoendelea Tanzania ikiwemo.
Kiteleja alisema, ugonjwa huo unashika nafasi ya pili kwa kusababisha saratani kwa wanawake huku ya kwanza ikiwa ni ya matiti lakini ndio inayoongoza kwa kusababisha vifo nchini ambapo kwa ujumla wa zote mbili husababisha vifo vyote vya kinamama kwa asilimia 50 vitokanavyo na saratani.
“Saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na virusi vya Papiloma (Human Papiloma Virus- HPV),huambukizwa kwa njia ya kujamiana katika umri mdogo,kuwa na wapenzi wengi,kuzaa watoto wengi na uvutaji wa sigara,” alisema Kiteleja.
Pia alisema, chanjo hiyo kwa mwaka huu itatolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 na baadaye itatolewa kwa Wote wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kabla ya kutolewa kwa miaka 9 pekee hawana budi kupata wakiwa na umri mdogo kabla hawajaambukizwa HPV kwani ni kinga na siyo tiba.
Vilevile alisema, chanjo hiyo itatolewa kwenye vituo vyote vinavyotoa huduma za afya ya mama na mtoto zikiwemo hospitali,vituo vya afya, zahanati na sehemu zinapotolewa huduma tembezi na huduma za mkoba hususani shuleni na bila malipo kwa wenye umri wa miaka 14 na itakuwa inatolewa kila siku baada ya hii leo kuzinduliwa.
Aidha alisema, ili kupata kinga kamili wanatakiwa wapate chanjo mara mbili, hivyo dozi ya pili inatakiwa wapatiwe baada ya miezi sita, jamii inapaswa kuelimishwa na kuhamasishwa umuhimu wa chanjo hiyo na kujitokeza kwa wingi ili kumaliza tatizo hilo kwa kina mama.
Na kuongeza kuwa kwa wenye umri wa miaka 15 na kuendelea wanaweza kupata chanjo hiyo katika hospitali binafsi ambapo watachangia gharama na njia ya kujikinga ni kutembelea vituo vya kutolea huduma za afya ya mama na mtoto mara kwa mara ili kufanyiwa uchunguzi wa kina na wataalam na ikibainika dalili za mwanzo kupatiwa matibabu stahiki.
Naye Afisa Chanjo wa Clinton Health Access Initiative Joan Mungereza alisema, chanjo hiyo ina gharama kubwa serikali kwa sasa kutokuwa na uwezo wa kuwapatia wote wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kwani kupitia Wizara ya Afya kwenye Mpango wa Taifa wa Chanjo una chanjo nyingi na zote zinatolewa bure hivyo mkakati na utoaji wa chanjo ni endelevu nchini katika kumaliza tatizo hilo kwa kina mama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.