Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima ameishauri Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira kukaa chini na kufanya tathmini makini kuhusiana na idadi halisi ya wakazi wa Jiji hilo ili miradi yake ya maji iwanufaishe wananchi wote.
Akizungumza na uongozi wa Mamlaka hiyo mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa chanzo cha maji Butimba,Mhe Malima amesema mara baada ya hesabu ya Sensa mwaka huu imeonesha Mwanza ina idadi ya watu milioni 4 hivyo mahitaji ya rasilimali hiyo itazidi kuwa kubwa.
"Nimemsikia hapa Meneja akisema mara baada ya mradi huo kukamilika utaweza kusambaza maji lita milioni 48 kwa siku hiyo haitoshi na Wananchi hawatawaelewa kuwa na mradi mkubwa namna hii halafu huduma ikawa bado hawaipati,ni lazima muone haja ya kufanya hesabu nzuri ili mradi huu uweze kutoa huduma kwa usahihi"amesema Mhe.Malima
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha bado wakazi wa Jiji la Mwanza hasa waishio maeneo ya kwenye miinuko wanataabika kupata huduma ya maji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa mtambo na maji kupotea njiani kabla ya kumfikia mwananchi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameutaka uongozi wa MWAUWASA kumletea taarifa ya kimaandishi kuhusiana
mradi huo kuchelewa kukabidhiwa tofauti na muda waliokubaliana ambao ni Disemba mwaka huu na sasa utakabidhiwa Juni mwakani.
"Alivyokuja Mhe.Makamu wa Rais Philip Mpango kuzindua mradi huu aliambiwa hadi Disemba utakuwa umekamilika,sasa leo mmnanipa taarifa tofauti yenye sababu zenu za msingi za vifaa kuchelewa kuletwa kutoka kwa msambazaji kutoka nje ya nchi".Amesema Mkuu huyo wa Mkoa
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,Mhandisi Leonard Msenyele amesema maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wameyapokea na kuyatekeleza ili malengo ya kuwapatia huduma bora wananchi yatimie.
Mradi wa chanzo cha maji Butimba upo chini ya mkandarasi SOGEA SATOM kutoka Ufaransa na umegharimu jumla ya Shilingi Bilioni 69.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.