MWENGE WA UHURU WARIDHISHWA NA UJENZI WA KITUO CHA AFYA NYAMAZUGO SENGEREMA
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava ameridhishwa na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamazugo wilayani Sengerema kinachotekelezwa kwa thamani ya Tshs. Milioni 500.
Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi leo Oktoba 07, 2024 kiongozi huyo amewapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri uliozaa mradi wenye ubora ukilinganisha na thamani ya fedha iliyotumika.
Ndugu Mnzava amesema Mhe. Rais ameamua kutoa fedha hizo kuwajengea wananchi wake zaidi ya 45,416 kutoka kwenye kata tatu za Nyamizeze, Kasenyi na Nyamazugo na maeneo ya jirani ili jamii iwe na uhakika wa kupata matibabu.
"Sengerema mmeitendea haki fedha iliyoletwa kwa ajili ya ujenzi huu, Mhe. Rais ameleta fedha hizi ili kuboresha huduma za afya, naomba muendelee kukamilisha ili kufika mwezi Disemba huduma zianze kutolewa." Amesema ndugu Mnzava.
Ujenzi wa kituo hicho cha afya uliibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona wanapata adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya na kwa awamu ya kwanza yanajengwa majengo ya wagonjwa wa nje, kufulia, maabara na wodi ya wazazi ya kisasa.
Aidha, Mwenge wa Uhuru umezindua mradi wa maji ya bomba katika kijiji cha Chifunfu wenye thamani ya Bilioni 2.9 fedha kutoka mpango wa maendeleo ya Maji (WSDP) uliotekelezwa na mkandarasi Emirate Builders Co. Ltd ambapo kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amewaagiza RUWASA kuongea vituo vya kutekea maji ili wananchi wote 31,423 katika vijiji vya Chifunfu, Lukumbi na Nyakahako wapate maji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.