MWENGE WA UHURU WAZINDUA MRADI WA KUKU WA MAYAI WA ZAIDI YA MILIONI 700 MISUNGWI
Leo Julai 18, 2023 Mwenge wa Uhuru umezindua mradi wa ufugaji kuku wenye thamani ya zaidi ya Milioni 700 katika kijiji cha Idetemia Usagara Wilayani Misungwi ambazo kati ya fedha hizo asilimia 65 ni mkopo toka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB).
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Abdalla Shaibu Kaim amempongeza mwekezaji (Angroberg Farm Ltd) kwa uwekezaji huo mkubwa na wa kisasa ambapo hadi sasa mradi huo una jumla ya kuku 20,000.
Ndugu Kaim amesema, kuamua kuwekeza fedha kubwa kiasi hicho ni dalili ya kuwa imara kimaono na ubunifu na hasa baada ya kukagua na kugundua kuwa mradi huo umezingatia usalama, afya na utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
"Huu si ufugaji tu bali ni wa kisasa, hongereni sana kwa ubunifu na uwekezaji mkubwa ambao umezingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira na kwa hakika Mwenge wa Uhuru umeridhika na ubora wa mradi." amesisitiza Ndugu Kaim.
Katika wakati mwingine Mwenge wa Uhuru umezindua madarasa aita kwenye shule ya Sekondari Idetemia yenye thamani ya zaidi ya Milioni 123 na kiongozi wa nbio za Mwenge wa Uhuru 2023 akatoa rai kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kuongeza usimamizi kwenye miradi hususani eneo la manunuzi ya vifaa.
Aidha, kutokana na dosari zilizobainika kwenye mradi huo Ndugu Kaim ametoa siku nne kwa wilaya hiyo kuhakikisha wanazirekebisha ili kuhakikisha kunakua na ubora ili wanafunzi wapate mazingira wezeshi kwa kujifunza na kujifunzia na kuongeza ufaulu kwenye shule hiyo.
"Mhe. Mkuu wa Wilaya endelea kusimamia miradi yetu ili ikamilike kwenye ubora hususani kwenye upande wa manunuzi ya vifaa hakikisha bei zinazingatia nyaraka za vifaa vya ujenzi (BOQ) ili fedha zitumike vizuri," amesema Ndugu Kaim, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023.
Baada ya ukaguzi wa kikundi cha wasafirishaji abiria (Bodaboda) Ngudama-Bulemeji Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye jengo la mionzi kwenye kituo cha afya Misasi na kuagiza usimamizi mzuri ili hatimaye iweze kukamilika kwa wakati lakini kwa ubora madhubuti.
Mwenge wa Uhuru umeipongeza Halmashauri ya Misungwi kwa kubuni mradi wa vibanda vya biashara kwenye stendi ya mabasi vinavyojengwa kwa zaidi ya Milioni 75 ambapo mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi na kubainisha kuwa utasaidia kuongeza mapato ya ndani na kujihakikishia kujitegemea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.