NAIBU WAZIRI KATAMBI AONYA WANAOVAMIA SHAMBA LA MIFUGO MABUKI
Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) amewataka wananchi wanaoishi karibu na Shamba la Mifugo la Mabuki wilayani Misungwi hususani jamii ya wafugaji kutovamia eneo hilo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya utafiti na ufugaji wa kisasa.
Ametoa agizo hilo leo Agosti 25, 2023 alipotembelea Shamba hilo na kuzungumza na Vijana 90 walio kwenye programu maalumu ya kuwajengea uwezo kiuchumi ambapo wananenepesha ng'ombe zaidi ya 900 kupitia vituo atamizi chini ya ufadhili wa Serikali.
Katambi amesema Serikali ya awamu ya Sita imeamua kurejesha hadhi ya shamba hilo lililoanzishwa na Rais Nyerere 1967 kwa kuwaletea vitendea kazi kama Matrekta mawili, Ng'ombe jike wa kisasa 500 pamoja na zaidi ya Milioni 650 kufadhili mradi huo nje ya mtaji na fedha za kujikimu wanazopewa vijana.
"Eneo hili ni lazima liheshimiwe kwani Serikali inawekeza kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wenyewe, naomba uongozi wa Shamba na Wilaya kwa ujumla tuendelee kuwaelimisha jamii inayozunguka shamba hili juu ya athari za uvamizi wao kwa maendeleo ya shamba hili." Amesisitiza.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imedhamiria kuwainua vijana kiuchumi na ndio maana imefanya maboresho kwenye Sera ya uchumi kwa vijana na kwamba siku za usoni itaanzishwa benki ya Vijana ambayo itawakopesha kwa dhamana ya maarifa yao.
Vilevile, ametoa wito kwa uongozi wa shamba hilo kutangaza soko la ng'ombe hao ili wauzwe na kununuliwa wengine na kunenepeshwa ili kukuza mitaji ya vijana hao waliotoka kwenye vyuo mbalimbali nchini na kuwezeshwa mitaji chini ya mpango wa Ujenzi wa Kesho bora (BBT) sekta ya mifugo.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Ndugu Emily Kasagara aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa ametumia wasaa huo kuishukuru Serikali kwa mradi huo na akaahidi kuwa serikali ya Mkoa itashirikiana na uongozi wa shamba hilo katika kudhibiti ufugaji haramu unaofanywa na baadhi ya wananchi.
Bi Lini Mwala, Meneja wa shamba hilo amefafanua kuwa uwepo wa shamba hilo lenye zaidi ya hekari elfu 25 umesaidia wananchi kupata elimu ya ufugaji na mbegu bora na kwamba kuna jumla ya ng'ombe 2742, mbuzi 356 na nyati maji 59 huku zaidi ya 50 wakiwa wameuzwa kwa wananchi kwa ajili ya kusambaza mbegu hiyo.
Meneja wa chuo cha mafunzo ya uvuvi Jacob Ngowi amesema kuwa tangia kuanzishwa kwa kituo hicho cha Uatamizi zaidi ya ng'ombe 165 wameuzwa na kwa wastani kila mmoja anakua na ongezeko la Kilogramu hadi 45 baada ya kunenepeshwa na ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Miundombinu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.