NAWAPONGEZA TMFD KWA KUCHAGUA KULIFANYIA KAZI ENEO LA UCHUMI WA BLUU: RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amekipongeza Chama cha Waandishi wa habari kuendeleza shughuli za bahari na uvuvi Tanzania TMFD kwa kuchagua kulifanyia kazi eneo hilo ambalo Serikali imelitengea shs bilioni 60 ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na tija.
Akizungumza Jumatatu hii kwenye kongamano la chama hicho lililofanyika kwenye ukumbi wa Mkutano Mwanza Hotel, Mkuu huyo wa mkoa amebainisha uamuzi wa kufanyia kazi eneo la uvuvi utachangia kuzidi kuimarika kwenye sekta hiyo na kuongezeka kwa ajira.
"Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya uvuvi Rais Samia ametoa shs bilioni 60 ambazo zimelenga kufanyika uvuvi wa kisasa ukiwemo ufugaji wa samaki kwa vizimba na boti za kisasa za uvuvi,sasa kalamu yenu imeongeza tija kwani mtafanya utafiti wa kina katika habari zenu na Serikali kuufanyia kazi,"Mhe.Mtanda.
Mkuu huyo wa mkoa amesema shughuli ya chama hicho itaunufaisha sana mkoa wa Mwanza ambao asilimia 53 ni maji ya ziwa Victoria,hivyo idadi kubwa wanaojishughulisha na uvuvi watafanya kazi zao kisasa zaidi.
"Mlichokifanya kwenye kongamano hilo ni kuishi kwenye maono ya Rais Samia ya kutoa fursa kupitia uchumi wa bluu,hatua hii ni jitihada nzuri za kumuunga mkono kiongozi wetu ambaye anataka kuona maendeleo ya kasi kwa wananchi.
Kwa upande wake mkurugenzi wa chama hicho Edwin Soko amesema wana mwaka mmoja na nusu tangu waanze shughuli zao lakini wanazidi kupata matokeo chanya kutokana na kuungwa mkono na Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali.
"Mhe Mkuu wa mkoa katika kuhakikisha tunafanya shughuli zetu kwa uhakika tuna utaratibu wa kuwajengea uwezo waandishi wetu na kutoa tuzo kwa wale wanaofanya vizuri,"
Sekta ya uvuvi kwa Mkoa wa Mwanza inachangia pato la mkoa kwa asilimia 7 wakati Taifa inachangia asilimia 1.8
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.