Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezitaka shule ya Sekondari Bwiru Wasichana na Sengerena Wavulana kuhakikisha hazipati tena daraja la nne na sifuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2020 kwa Serikali imetatua changamoto zilizokuwapo kwa asilimia 90.
Kauli aliitoa mkoani Mwanza kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hizo katika ziara yake ya kukagua na kupokea majengo ya shule kongwe nchini ambazo zimefanyiwa ukarabati na ujenzi mpya wa miundombinu uliogharimu Sh bilioni 19.2.
Akiwa Bwiru Wasichana iliyopo Wilaya ya Ilemela, Profesa Ndalichako alisema shule hiyo imefanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu ambapo hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la sifuri, hivyo imejisikia faraja na kuona anastahili kuendelea kuongoza sekta ya elimu.
“Bwiru mmenibeba juu kwa kile mlichofanya katika matokeo ya mwaka huu kidato cha sita, ni ushindi mkubwa na sitaki kusikia tena mnapata daraja la sifuri au la nne, hakikishe kwa sababu changamoto zilizokuwapo zimetatuliwa kwa kiasi kikubwa, kazi imebaki kwa watumishi na wanafunzi kutumia miundombinu iliyobereshwa kutimiza wajibu wenu.
“Naomba niagize kabisa wakurugenzi kwamba walimu wa shule zilizofanya vizuri ikiwamo Bwiru hakikisheni mnawapandisha madaraja walimu wote wenye sifa na walipwe stahiki zao za likizo zao.Pia pongezi hizo ziende kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa namna walivyoiwakilisha Serikali katika kusimamia ukarabati wa shule kongwe,”alisema.
Awali akitoa taarifa ya taaluma, Mkuu wa Shule ya Bwiru, Mecktilda Shija alisema katika matokeo ya mwaka 2018 wanafunzi 33 walipata daraja la kwanza, daraja la pili walikuwa 198, la tatu 196, la nne walikuwa 17 na sifuri walikuwa wanne.
“Katika matokeo ya mwaka huu 2019, tumefanya vizuri zaidi kwani ya kati ya watoto 404, daraja la kwanza walikuwa 78, daraja la pili wlaikuwa 154, daraja la tatu walikuwa 163 na daraja la nne walikuwa watano na hatukuwa na sifuri, hivuo lengo letu mwaka 2020 hatutakuwa na darala la nne,”alisema Shija.
Kwa upande wa Mkuu wa Shule ya Sengerema, Zacharia Kahema alimweleza Profesa Ndalichako kwamba katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2018 daraja la kwanza kulikuwa na wanafunzi 56, daraja la pili wanafunzi 243, daraja la tatu wanafunzi 266, darala la nne wanafunzi 120 na sifuri walikuwa wawili.
“Matokeo ya mwaka huu yalikuwa mazuri zaidi kwani daraja la kwanza wnafunzi 72, daraja la pili wanafunzi 551, daraja la tatu wanafunzi 214, daraja la nne wanafunzi watano na sifuri alikuwa mmoja tu, pamoja na mafanikio hayo tunaomba msaada wa kupatiwa gari kwa ajili ya shule ambalo litatusaidia katika shughuli za shule,”alisema.
Hata hivyo Profesa Ndalichako aliwataka walimu na wanafunzi kuwasaidia kwa namna moja au nyingine baadhi ya wanafunzi ambao wanaonekana ni wazito kuelewa ili kufuta daraja sifuri maana wanasababisha shule kushuka kutoka nafasi za juu.
“Kwa kweli nafarijika kuona shule za Serikali zikifanya vizuri, hawa wanafunzi mmoja au wawili wanaopata daraja la sifuri kwa kweli naomba mkiwagundua mapema wana uelekeo wa kupata daraja hilo wasaidieni kwa namna moja au nyingine, walimu na wanafunzi wenzao mlikuwa na nafasi ya kuwainua ili kufuta sifuri hiyo,”alisema Profesa Ndalichako.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alimhakikishia waziri huyo kwamba miundombinu iliyoboreshwa itatunzwa huku akiwataka watumishi na wanafunzi kutambua wana deni kubwa sana la kutumia rasilimali hizo kuleta matokeo bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.