Washiriki wa chuo cha taifa cha ulinzi leo Januari 23, 2026 wamehitimisha ziara ya mafunzo ya siku tano Mkoani Mwanza waliyoifanya katika maeneo mbalimbali mathalani kwenye miradi ya maendeleo ambayo wameitembelea kuona namna gani inatekelezwa.

Akizungumza kwenye hafla ya majumuisho Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameishukuru timu hiyo kwa ziara yenye tija ndani ya Mkoa na amewaahidi kufanyia kazi ushauri walioutoa katika kuboresha huduma.

Akizungumzia eneo la mipango miji, Mhe. Mtanda amebainisha mipango ya serikali ya kuwajengea wajasiriamali miundombinu rafiki ya kufanyia biashara ili wawe kwenye mazingira nadhifu na yenye tija kwao.

“Tutawasiliana na wizara ya Maliasili na Utaliii kuona namna ya kushirikiana nao kwenye kuongeza elimu kwa umma juu ya kutangaza vivutio vya utalii na kuweka mikakati ya kushirikiana na wadau kukuza sekta hiyo.” Mhe. Mtanda.

Naye, kiongozi wa timu hiyo Brigedia Jenerali Matunda amesema ziara yao imezaa matunda kwani wamepata walichokikusudia na wamejifunza mbinu, teknolojia na utekelezaji wa miradi kwa ujumla jinsi bavyo serikali inafanikisha.

Amesema, wamejionea kwa macho jinsi ambavyo serikali ya Tanzania imewekeza fedha nyingi kwenye miradi katika sekta za miundombinu, kilimo, utalii, uvuvi, ufugaji na viwanda jambo linaloipa nchi uhakika wa mazao na uzalishaji na kupelekea uhakika wa usalama wa chakula kwa wananchi wake.

Aidha, wameipongeza serikali kwa kuwajengea uwezo vijana kutumia mbinu za kisasa hususani kwenye ufugaji wa kisasa wa kuku na teknolojia ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unaofanywa na makundi ya vijana ambao unasaidia kuhifadhi mazingira na kulinda mazalia ya samaki katika ziwa Victoria.

Pamoja na kupongeza kwenye uimarishaji wa usafiri katika ziwa kwa kujenga kituo cha uokozi na meli ya kisasa, wanafunzi hao wa vitendo wamebainisha changamoto kadhaa ikiwemo ukatishaji wa safari za ndege ambao wamehimiza kurekebishwa ili kutoikosesha serikali fedha kutokana na kodi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.