ONGEZENI BIDII DIMBANI ILI TUSHINDE MICHEZO MITATU ILIYOBAKI, EPUKENI HUJUMA: RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo amejumuika kwenye mazoezi ya timu ya Pamba Jiji FC kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana na kuwataka kukaza buti michezo yote mitatu iliyobaki ya ligi ya Championship na kuonya kusiwepo na aina yoyote ya usaliti kwa timu.
Mkuu huyo wa Mkoa aliyetinga uwanjani na kupasha mazoezi amesema michezo iliyobaki waipe uzito na kutoka na ushindi wa kishindo hasa kutokana na kupishana pointi chache na wanaonyemelea nafasi ya kupanda.
"Nawaahidi motisha zote zipo palepale alipoishia mtangulizi wangu mimi napaendeleza nimezungumza na uongozi wenu hivyo wajibu uliopo mbele yetu ni kushinda tu tukianzia mchezo wa kesho dhidi ya PGA Talent", RC Mtanda.
Aidha, Mtanda amewaonya wachezaji hao wasithubutu kujiingiza katika mchezo mchafu wa kuihujumu timu na atakayebainika hatosita kumchukulia hatua.
"Ni lazima mtambue tupo katika nafasi nzuri ya kupanda ligi kuu na pia mjihadhari na fitna zinazoweza kujitokeza ili tukwame katika malengo yetu," amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa aliyechezea timu ya Bunge.
Kocha Mkuu wa Pamba Jiji FC Mbwana Makatta amesema hana shaka na kikosi chake na kasoro zote za kiufundi zilizojitokeza wamezifanyia kazi.
"Mhe. Mkuu wa mkoa tumefarijika sana kuwa nawe na hasa kujumuika nasi katika mazoezi tumejiona ni mwenzetu haswa, sisi maelekezo yako yote tunayafanyia kazi ili tutimize ndoto ya kupanda ligi kuu msimu ujao,"Makatta
Mhe. Mtanda pia alitoa nafasi kwa mchezaji wa zamani wa timu hiyo Fumo Felician kutoa nasaha kwa wachezaji hao ambaye aliwakumbusha kutambua matarajio ya wana Mwanza ya kupata burudani ya ligi kuu kwa timu yao ya nyumbani waliyoikosa kwa miaka mingi.
Pamba Jiji FC maarufu kama TP Lindanda wakiwa na pointi 58 nafasi ya pili, watashuka dimbani Nyamagana Jumamosi hii kumenyana na PGA Talent kutoka Ruvuma kabla ya kufunga safari mkoani Arusha kuhitimisha michezo miwili na TMA Aprili 21 na siku saba baadaye dhidi ya Mbuni FC.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.