Rais Dkt .John Magufuli ametimiza ahadi yake aliyoitoa mwezi juni mwaka jana ya kuwapa pikipiki maofisa tarafa nchini ambapo pikipiki 24 aina ya Sanlg zimekabidhiwa kwa maafisa tarafa wa Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi kwa maafisa tarafa hao.
Akikabidhi pikipiki hizo kwa niaba ya Mhe. Rais Magufuli Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella aliwataka maafisa tarafa hao kuzitumia pikipiki hizo kwa shughuli za Serikali zilizokusudiwa na kuzingatia maadili ya kazi katika maeneo yao ili kuleta maendeleo kwa wananchi .
“ Rais amewaamini Maofisa Tarafa akaamua kuwapa nyenzo hizo ambazo ni mali ya Serikali kwa ajili ya kuondoa kilio cha usafiri,hivyo mzitunze kama mnavyotunza ofisi na nyaraka nyingine,sijawai kusikia sifa mbaya kwa Maofisa hawa wa Mkoa wangu,sitegemei baada ya kupatiwa chombo hiki cha usafiri ndiyo hadithi zianze nachotarajia pikipiki hizi zitumike kwa matumizi yaliyolengwa ya kusimamia ulinzi na usalama wa wananchi kwa kutunza watu na mali zao,kuhamasisha maendeleo na kusimamia maendeleo ndiyo kazi yenu kubwa.”alisema Mhe. Mongella.
Aidha Mhe. Mongella ameongeza kuwa usafiri huo utawafanya wafike kila eneo kwa urahisi zaidi na kuchochea kasi ya maendeleo.
"Nategemea nikifika kwenye tarafa nikute amsha amsha ya maendeleo,kwa sababu mtakuwa hamjachoka mkitoka eneo moja kwenda vijiji vitatu vinne mnakagua kisha mnarudi baada ya hapo mnaenda tena vijiji vingine ambapo mnapaswa kuwa na mpangilio mzuri wa kazi,hivyo mwaka huu kuna kazi nyingi za maendeleo mhakikishe mnazifanya na uchaguzi mkuu unakuja mtimize wajibu wanu, alisisitiza."
Hata hivyo pamoja na msisitizo mkubwa Mhe. Mongella alioutoa,alifafanua kuwa maofisa hao ni kiungo kikubwa katika maendeleo kwani wapo katika kazi zote(all functions) ambapo kwenye kazi za maendeleo na ulinzi, usalama wa maendeleo pia,ukienda kwenye Wilaya mtu anayefanya kazi katika ofisi zote mbili za Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya ni Maafisa Tarafa vyo ni tegemeo kubwa katika Shughuli za kila siku.
"Rais ameisha toa pikipiki,tusimuangushe ametutendea jambo jema,kwahiyo mimi nawaachia nyiye nendeni mkafanye kazi kwa kushirikiana,msianze kufanyia ujasiriamali na hizi pikipiki lisije likatokea hilo tukio,kwamba sasa unakuta mwanadada,Afisa Tarafa hawezi kuendesha katafuta kijana, pikipiki ya Afisa Tarafa ipo kijiweni inasanya ni marufuku tafadhali sana zitumike kwa malengo yaliyo pangwa, nategemea kwa nyenzo hizi ufanisi utakuwa maradufu,"alisema Mongella.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Emmanuel Tutuba, akitoa mchanganuo wa namna pikipiki hizo zitakavyogawanywa kwa maafisa tarafa wa wilaya za mkoa huo alisema, Mkoa huo umepokea jumla ya pikipiki 24 ambazo wamegawiwa Maofisa Tarafa wote ambapo Wilaya ya Kwimba tarafa 5, Sengerema 5,Magu 4,Misungwi 4, Nyamagana 1, Ilemela 1 na Ukerewe 4.
" Pikipiki hizi ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Mhe.Dkt.John Magufuli katika kikao cha Juni 4,2019 kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya Maafisa Tarafa kuomba kupatiwa usafiri ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa wakati ambapo kila Afisa Tarafa amepewa pikipiki hii Kama chombo cha usafiri kwa shughuli za Serikali katika eneo lake la kazi," alisema Tutuba.
Naye Afisa Tarafa Ukara Wilayani Ukerewe James Chuwa, alimshukuru Mhe. Rais kwa kuwapatia pikipiki hizo ambazo zitawasaidia katika usafiri na kudai kuwa awali wamepitia kipindi kigumu katika kuwafikia wananchi wa chini kabisa pamoja na kutatua matatizo yao ilikuwa lazima watumie fedha zao za mfukoni kwa ajili ya usafiri kwa ajili ya kutatua kero za wananchi.
"Ila sasa hivi tunamuahidi Mhe. Rais kwa vile ameishatupatia vyombo vya usafiri na tuna uhakika wa kufika field(eneo husika) ili kutatua kero za wananchi,sasa mabango hatoyaona tena,lakini jambo jingine la kumshukuru Mhe. Rais tunakwenda kufanya kazi kama ambavyo yeye alituahidi usafiri na sisi sasa tumeisha pokea na tunaenda kutenda kazi sawa sawa," alisema Chuwa.
Kwa upande wake Afisa Tarafa Mbarika Wilayani Misungwi Cresensia Mwalongo, alisema kupitia pikipiki hizo,zitawasaidia kwa kuwafikia wananchi na kutatua kero zao kwa wakati,nyuma walikuwa wanaletewa kesi ila ukiangalia ni kwa namna gani ya kufika eneo la tukio ilikuwa inawapa wakati mgumu ambapo pia wanajifunza kuendesha vyombo hivyo vya usafiri ili waweze kuvitumia kama ilivyokusudiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.