Rais.Dkt. John Magufuli amezindua miradi saba katika Hospitali ya Kanda ya Bugando ya jijini Mwanza yenye thamani ya Sh bilioni 15 huku akimwagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuanza kufuatilia na kuthibisha uhalali kama viongozi wote waliokwenda kutibiwa nchini India walikuwa wanaumwa au la.
Mhe.Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo jijini Mwanza wakati azikindua miradi saba katika Hospitali ya Kanda ya Bugando.
“Hii nchi ni tajiri sana isipokuwa ilikuwa inaliwa na mafisadi na mimi nimejitoa uhai wangu kwa ajili ya kupambana nao, wengine walikuwa wanakwenda India hata kutibiwa mafua, haitoshi walikuwa wanaambatana na wake zao au waume zao, nao wakifika huko anaulizwa kama aingizwe kwenye malipo.
“Yaani Mgonjwa na msindikizaji wote wanaingizwa katika malipo na gharama zote hizo zilikuwa zinaletwa Tanzania ilipe, nasema Waziri kafuatilie huko kama utakuta wengine hawakupata kibali cha kutibiwa huko, fedha hizo watalipa wenyewe na hazitalipwa na Serikali, nimesema na wanaosikia wasikie na wasiosikia na wasisikie,”alisema.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameitaka Wizara ya afya kufanya utafiti sababu ya watanzania asilimia zaidi ya 50 wanaugua saratani na moyo huku akielekeza hatua zichukuliwe haraka.Alisema inawezekana wananchi hao wanapatwa na maradhi hayo kutokana shughuli mbalimbali za uchimbaji wa madini unaofanyika na kutiririsha sumu kwenye maji.
Pia amewataka wakurugenzi wa Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kutenga Sh. bilioni 4 kwa ajili ya kujenga jengo la abiria katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mwanza kwa kutumia force account huku akimtaka Mkuu wa Mkoa Mhe. John Mongella kusimamia hilo.
Katika hatua nyingine, Mhe.Rais Magufuli ametoa ahadi ya Sh.milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana na bwalo katika Shule ya Sekondari ya Mwanza. Ahadi hiyo ameitoa wakati aliposimama eneo la shule hiyo na kuongea na wanafunzi hao.
Vile vile amesema ujenzi wa daraja la Busisi linalounganisha Wilaya ya Misungwi na Sengerema lenye urefu wa kilomita 3.2 litaanza kujengwa hivi karibuni ili kuwaondolea adha wananchi ambao wanataka kuvuka.
Naye Profesa Abel Makubi Mkurugenzi wa Hospitali ya kanda ya Bugando akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo,amesema kwa kipindi cha miaka minne wamefanikiwa kuboresha huduma za afya na kukamilisha miradi saba ambayo ni kitengo cha saratani, mahututi, upasuaji, oksijeni na viwanda vidogo ambavyo vitakuwa vinazalisha dawa kwa ajili ya wagonjwa.
Ameongeza kuwa asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani ambao walikuwa wanakwenda katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam walikuwa wanatoka Kanda ya Ziwa, hivyo imewapunguzia gharama na usumbufu wa kusafiri kutafuta huduma hiyo.
Ameongeza kuwa hivi sasa asilimia 65 ya wagonjwa waliokuwa wanakwenda katika hospitali ya Ocean Road wanatibiwa Bugando.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu amesema wamefanikiwa kudhibiti na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa mwezi kutoka Sh. bilioni 1.2 mwaka 2016 hadi Sh. bilioni 3.9 mwaka huu.
“Kama Serikali tumeendelea kushirikiana na Bugando ambapo kwa mwaka tumekuwa tukitoa Sh 1.6 bilioni kwa ajili ya kuwalipa mishahara ya watumishi kila mwezi, vile vile kila mwezi tunatoa Sh. bilioni moja saratani kwa ajili ya dawa za saratani, lengo ni kuwapunguzia gharama wananchi maana mgonjwa mmoja alikuwa akitakiwa kutoa Sh.300,000 hadi 400,000.
“Serikali tumeendelea kutenga fedha ambapo hivi sasa tumetoa Sh bilioni 1.7 kwa ajili ya kujenga wodi ya wagonjwa, pia katika Mkoa wa Mwanza tunatoa dawa za Sh bilioni 7.9 mwaka huu kutoka Sh bilioni 1.2 mwaka 2016, kwa kutambua umuhimu wa huduma za afya watu wa kanda ya ziwa tunajenga jengo la mama na mtoto pale hospitali ya Mkoa –Sekoutoure,”alisema Mhe. Mwalimu.
Hata hivyo ameongeza kuwa Serikali imefunga mashine mpya za kisasa katika vituo vya damu zenye thamani ya Sh bilioni 13.2 kwa ajili ya maradhi ya damu lengo likiwa ni kupata damu salama katika mikoa ya Kanda Ziwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.