Rais mstaafu, Mhe.Benjamin Mkapa ameishauri Tume ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuvishirikisha vyuo binafsi katika majadiliano yoyote pale inapokusudia kufanya jambo lolote juu ya elimu ya juu, kwani kufanya hivyo kutaondoa malalamiko dhidi yao na kuleta uwazi.
Ushauri huo aliutoa jijini Mwanza katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) ambapo Mhe. Mkapa alisema TCU ambayo ndiyo mdhibiti mkuu wa elimu ya juu na mshauri wa serikali inapaswa kufanya kazi kwa ukaribu na vyuo binfasi.
Alisema TCU yapo malalamiko mengi kutoka vyuo binafsi juu ya uminywaji wa uhuru kutokana na uwepo vya sheria kadhaa jambo ambalo linazorotesha ustawi vya vyuo binafsi hususani vile vichanga, hivyo alishauri tume hiyo kuongeza ushirikishwaji kwa kila hatua ili kuijenga Tanzania yenye usawa katika elimu.
“Miaka 20 ya SAUT si mchezo, nawapongeza sana kwa kazi mliyofanya ya kutoa elimu bora na tunashuhudia baadhi ya viongozi wa Serikali wamepitia hapa, hapa Tanzania tunavyo vyuo 48 ambapo 15 ni binafsi hivyo binafsi naomba kushauri TCU isiwe na sheria za kuminya uhuru wa vyuo binafsi.
“Washirikishwe kwa kila hatua katika mapendekezo yote maana bila vyuo binafsi hatuwezi kusema Serikali itatosheleza kwa kila kitu, niwahakikishie SAUT fanyeni kazi yenu mkiwa kifua mbele jisikieni nyinyi ni miongoni mwa vyuo bora Tanzania kwa kuwa matunda yake yanaonekana lakini kubwa zaidi vyuo vya Serikali navyo vinapaswa kushirikiana na binafsi,”alisema.
Hata hivyo Mhe. Mkapa aliweza kutoa pongezi kwa uongozi wa SAUT kutokana na kazi kubwa waliyofanya tangu mwaka 1998 kwa kupanua chuo hicho na kuanzisha vitivo kadhaa ambapo kwa pamoja maendeleo yamepatikana huku akisisitiza kwamba malengo waliyojiwekea ya miaka mitano ijayo yatafanikiwa kwa kuwa tayari wamejenga msingi imara.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Mhe.Profesa Costa Mahalu aliishukuru Serikali kwa kushirikiana katika utoaji wa elimu ya juu huku akiomba kushirikishwa kwa baadhi ya mambo kabla ya kutoa maelekezo kwa vyuo vikuu.
Profesa Mahalu ambaye alijikita sana kueleza historia ya chuo hicho huku akiwataja viongozi wengi wa Serikali na wabunge walisoma SAUT akiwamo Waziri wa Madini, Mhe. Dotto Biteko, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti kwamba ni matunda ya chuo hicho.
Pia aliwataja, John Heche, Ezekiel Wenje, Moses Machali, Zamaradi Kawawa na wengine wengi ambapo alisema huo ni mfano kwamba SAUT inawaandaa wasomi ambao wanaonekana ndani ya jamii na mamlaka za uteuzi huku akisisitiza hiyo ni kutokana na mfumo unaotumika kuwaandaa kimaadili.
Profesa Mahalu alimshukuru Mkapa kwa kuwajengea lami kutoka barabara kuu ya Mwanza –Shinganya hadi chuoni hapo na kumtolea mfano kama kiongozi wa kwanza kuruhusu wanafunzi wa vyuo binafsi kupata mkopo kutoka serikalini wakati wa utawala wake.
“Kikubwa ni kuiomba na kuishauri Serikali na sekta binafsi kuwatumia wasomi mbalimbali katika mipango ya maendeleo ya nchi ili wananchi waweze kufaidika na matunda ya usomi wao, hivyo Serikali ivishirikishe vyuo binafsi katika majadiliano ya mipango sekta ya elimu badala ya kujifungia wenyewe,”alisema Profesa Mahalu.
Naye Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo la Geita Mhasham Flaviana Matindi, alisema wahitimu wengi wa vyuo vikuu wanapohitimu huwa wana mawazo ya kupata ajira lakini ndani ya chuo hicho wamewajengea misingi ya kujiamini na kujiajiri.
“Miaka mitano ijayo tumejiwekea malengo ya kutengeneza tunu, hatutaki kuwa na majengo makubwa ambayo hayaendani na ujuzi tunaoutoa ndio maana tumeagiza kila kitivo kwa kila mwezi ni lazima kijitathmini ili kujua mapungufu yao na kuyafanyia kazi, kwa miaka hiyo ijayo tunataka kuwa na tunu kila kitivo,”alisema.
Kwa upande wake Waziri wa madini Mhe.Doto Biteko,alisema ni wakati muafaka kwa watanzania kutoka katika misingi ya kulalamika na kwenda misingi ya vitendo ambapo alisisitiza kuwa kwa utawala wa sasa hautoi mwanya kwa kijana kusubiria kushikwa mkono ili kupata ajira, kila mmoja anatakiwa kuonyesha uwezo wake.
Pia alisema anafarijika kuona akiwa waziri wa madini huku akiwa na kumbukumbu ya kuwa Rais wa Serikali ya wanafunzi wa SAUT enzi hizo akiwa anasoma hapo ambapo alidokeza kuwa baraza lake aliloliteua, nao pia ni viongozi wa Serikali na wabunge kwa sasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.