RAIS SAMIA AONGOZA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE WA UHURU MWANZA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 14, 2024 amewaongoza watanzania katika kilele cha kishindo cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 sherehe zilizofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba uliopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Akiongea na wananchi Mhe. Rais amewataka watendaji katka Halmashauri zote nchini kutekeleza miradi kizalendo kwa kuzingatia sheria na kanuni na katika kuwainua vijana amebainisha kuwa umefika wakati sasa kwa halmashauri nchini kununua vifaa kutoka kwenye kundi hilo ili kuwainua kiuchumi kwa kuongeza kipato.
Akitoa risala kwa Mhe. Rais, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 Godfrey Mnzava amesema wananchi kote nchini wametoa salamu za pongezi kwa Serikali kwa kuboresha huduma za kijamii kama maji, elimu, afya pamoja na miundombinu ya barabara na wameomba kuboreshewa sehemu chache zenye changamoto.
Aidha, amebainisha kuwepo kwa kasoro kwenye miradi 16 kati ya zaidi ya miradi 1500 ambayo Mwenge wa Uhuru umetembelea mwaka huu na kwamba TAKUKURU wamegizwa kufuatilia nyaraka za miradi hiyo ili waliohusika kufanya ubadhirifu wachukuliwe hatua ikiwemo kutofuata taratibu za manunuzi ya umma.
"Pamoja na ukaguzi wa miradi, kupitia mikesha lita 5,832 za damu zimekusanywa kutokana na uchangiaji wa wananchi ambazo zitasaidia wahitaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini." Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Mwenge wa Uhuru mkoani humo umefika kwenye miradi 53 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 99 na akabainisha kuwa asilimia 30 ya wananchi wamejiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mnamo novemba 27, 2024.
Hali kadhalika Rais Samia amemkabidhi Mwenge wa Uhuru na Bendera Mkuu wa majeshi ya ulinzi JWTZ ,Jenerali Jacob Nkunda ili ukapandishwe kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro kama ishara ya kutimiza miaka 60 tangu kupandishwa hapo juu
Mwenge wa Uhuru umekagua nchi nzima miradi yenye thamani ya shs trilioni 11
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zilianza mkoani Kilimanjaro kwa kuzindua mradi wa sekta ya Elimu kwenye manispaa ya Moshi tarehe 02 Aprili, 2024 na kuhitimishwa jana katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela-Mwanza kwa kuzindua ujenzi wa barabara ya lami nzito (Asphalt Concrete) ya Kiyungi (0.49).
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu uliokagua miradi ya jumla ya shs trilioni 11 nchi nzima, "Tunza mazingira na shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.