RAIS SAMIA AWASILI MWANZA KWA ZIARA YA KIKAZI
*Awaahidi Watanzania kuwaletea maendeleo*
*Awataka wananchi kulinda Mila na Tamaduni*
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Juni 12, 2023 amewasili Mkoani Mwanza kwa ziara ya Kikazi ambapo kesho jumanne anatarajiwa Kuwa Mgeni Rasmi kwenye Tamasha la Ngoma za Kabila la Wasukuma (Bulabo) kabla ya Kukagua Miradi ya Maendeleo ya Kimkakati siku ya Jumatano.
Akiwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki kwenye Uwanja wa Ndege jioni hii Mhe. Rais amewahakikishia Watanzania kuwa yeye kama kiongozi Mkuu wa nchi siku zote ataendelea kuwalinda wananchi wake na daima atawaletea maendeleo na si vinginevyo.
"Tanzania ni moja na daima nitasimamia Maendeleo, kila linalofanyika ni kwa maendeleo yetu sote na haiuziki nchi hii wala kugawiwa kwa mtu yeyote." amefafanua Dkt. Samia.
Aidha, Rais Samia amewataka wananchi kuenzi Mila na tamaduni za mababu ili kuwa na urithi endelevu kwa kuwa nchi yoyote lazima iwe na mila zake.
"Mwanza ndiko nilikokabidhiwa Uchifu na Uhangaya hivyo nimekuja kwenye sherehe zetu za kutunza mila na tamaduni zetu na kwa sasa tuna tamasha la kutimiza miaka miwili."
Akimkaribisha Mhe. Rais, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amemhakikishia Usalama ndani ya Mkoa huo na amebainisha kuwa watu wake wana imani kubwa na maendeleo yanayochagizwa na Uongozi wake thabiti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.